AFRIKA
2 dk kusoma
Jela kwa wasafirishaji wa siafu Kenya
Miongoni mwa wanne hao kuna raia wawili wa Ubelgiji ambao walipatikana na hatia kwa kujaribu kusafirisha siafu hao adimu nje ya nchi.
Jela kwa wasafirishaji wa siafu Kenya
Watu wanne wamehukumiwa nchini kenya kwa kusafirisha siafu kinyume na sheria . Picha: Reuters / Reuters
7 Mei 2025

Mahakama ya Kenya iliwahukumu watu wanne siku ya Jumatano, wakiwemo vijana wawili wa Ubelgiji, kifungo cha mwaka mmoja jela au faini ya zaidi ya dola 7,000 kwa kujaribu kusafirisha maelfu ya siafu adimu walio hai nje ya nchi.

Shirika la Huduma ya Wanyamapori nchini Kenya (KWS) limewashutumu wanne hao kwa kujihusisha na "uharamia wa kibayolojia" kwa kujaribu kusafirisha siafu hao adimu nje ya nchi.

David Lornoy na Seppe Lodewijckx, wote wenye umri wa miaka 18 kutoka Ubelgiji, Duh Hung Nguyen wa Vietnam na Dennis Nganga wa Kenya wote walikiri kuwa na wqdudu hao, lakini walikana kutaka kusafirisha siafu.

Lornoy na Lodewijckx walikamatwa wakiwa na siafu 5,000 wakiwa wamewaweka katika sehemu ndogo ndogo 2,244 Kaunti ya Nakuru, karibu kilomita 160 kutoka mji mkuu wa Kenya,Nairobi.

Duh na Nganga walikutwa na siafu wakiwa wamehifadhiwa kwenye mabomba ya sindano 140 yaliyowekwa pamba na makontena mawili.

Kesi hizo mbili zilikuwa tofauti lakini zote nne zilisikilizwa kwa pamoja.

Kumiliki nyara bila kibali ni kosa la jinai nchini Kenya, na washukiwa walikuwa wanakabiliwa na faini ya hadi dola 10,000 na kifungo cha miaka mitano au zaidi.

Bei za rejareja nchini Uingereza zinaonesha kwamba bei ya wadudu hao inaweza kufikia dola milioni 1 barani Ulaya, ambapo wenyewe huhifadhi siafu katika vyombo vikubwa vya wazi vinavyojulikana kama ‘formicariums’ na kutathmini mienendo yao.

Mahakama siku ya Jumatano ilisema washukiwa hao wanaweza kukaa gerezani mwaka mmoja au kulipa faini ya shilingi milioni moja ya Kenya (dola 7,740), ambayo ndiyo thamani iliyokadiriwa na polisi ya siafu hao.


Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us