Katika taarifa yao Jumatatu, KWS imesema faru huyo dume mweusi alionekana akiwa na mama yake siku chache zilizopita. Sasa idadi ya faru weusi imefika 23 nchini Kenya.
“Tunafurahi kutangaza kuzaliwa kwa faru mwingine mweusi katika eneo la hifadhi la Sera. Maafisa wa KWS pamoja na wafanyakazi wa Sera wanaofuatilia masuala ya faru,walimuona faru mama na mwingine mdogo dume siku chache zilizopita. Huu ni ushindi kwa tunaofanya shughuli za hifadhi za wanyamapori’’ Shirika hilo lilisema katika taarifa.
Mwezi Oktoba mwaka jana, faru mwingine mweusi alizaliwa katika moja ya hifadhi.
Farua mweusi ni aina ambayo imetia hofu kwa wahifadhi wa wanyamapori kutokana na kupungua kwa idadi yake.
Katika miaka ya themanini idadi ya faru hao ilikuwa karibu 20,000. Ujangili na biashara haramu ya meno yao ukasababisha idadi yao kupungua hadi 400 mwaka 1987.
Bado ujangili unachangia katika kuhatarisha idadi yao na kutatiza juhudi za kurejesha faru katika sehemu salama.
Kwa ujumla Kenya ni ya tatu barani Afrika kwa idadi kubwa ya faru baada ya Afrika Kusini na Namibia.
Afrika Kusini ina faru karibu 15,000 huko nchini Namibia wanyama hao wakisemekana kuwa 3,390 na katika taifa la Kenya idadi ya faru ikiwa 2,021.