Anajulikana kama Vee Money, ila cheti chake cha taifa anasomeka kama Vanessa Mdee.
Vanessa Mdee, aliyejaliwa sauti nyororo na sura ya kuvutia, alizaliwa Juni 7, 1988 mkoani Arusha nchini Tanzania.
Alianza kujihusisha na tasnia ya burudani akiwa bado ni mwanafunzi wa sheria jijini Nairobi, nchini Kenya, ikiwa ni miezi michache tu toka kutokea kwa kifo cha baba yake.
Safari ya sanaa
Uamuzi wake wa kujihusisha na shindano la kumtafuta mtangazaji wa kituo cha burudani cha MTV ulianzisha rasmi safari yake ya kuingia kwenye tasnia ya burudani.
Alianza kama mtangazaji wa kituo cha redio cha Choice FM nchini na kumfanya kuwa maarufu kati ya wasikilizaji wa kituo hicho ambacho ni sehemu ya Clouds FM.
Alisikika kwenye wimbo “Money” aliofanya na msanii, japo haukupata umaarufu, kabla ya kuja kuibuka na kwenye kolabo na Ommy Dimpoz kwenye "Me and You" iliyotoka mwaka 2013 na kukonga nyoyo za wapenda burudani Afrika Mashariki.
Mwaka 2014, Vanessa Mdee alitoa albamu yake ya kwanza iitwayo "Closer," iliyokuwa na mahadhi ya R&B na Bongo Flava.
Ngoma kama "Nobody But Me," "Niroge, "Game", na nyingine nyingi ziliifanya nyota ya Vanessa Mdee izidi kung’ara Afrika Mashariki.
Katika kukuza sanaa yake, mwaka 2017, Vanessa Mdee alianzisha lebo ya muziki iitwayo Mdee Music na mwaka mmoja baadaye kuachia albamu iitwayo "Money Mondays," iliyokuwa na ngoma kama "Kisela," "Juu" na "Wet".
Vanessa Mdee ndiye msanii pekee Afrika Mashariki na Kati kufanya tour ya nchi nzima, akiwa pamoja na msanii mwenzake aitwaye Jux.
Nje ya muziki, Vanessa Mdee amewahi kuwa mtangazaji wa kipindi cha "The MTV Base Meets" na aliwahi kuwa mkufunzi wa “East Africa’s Got Talent.”
Pia, amewahi kushiriki kwenye msimu wa 5 wa “MTV Shuga: Down South”, akishiriki kama mke wa tajiri muhuni.
Ushirikina kwenye muziki
Mwaka 2020, Vanessa Mdee alitangaza rasmi kuachana na tasnia ya muziki, akitoa sababu za changamoto ya afya ya akili, akiongeza kuwa suala la ushirikina limekuwa likuhishwa na tasnia hiyo.
Mwaka huo huo, aliingia kwenye mahusiano ya kimapenzi na muigizaji kutoka Nigeria mwenye uraia pia wa Marekani, Olurotimi Akinosho, maarufu kama Rotimi.
Wawili hao wamejaliwa kupata watatu na kwa sasa anaishi Afrika Kusini.
Vanessa Mdee ni ndugu ya wasanii Mimi Mars na Nancy Namtero Tero Mdee.