Ghana imepokea kundi la kwanza la raia wa Afrika Magharibi waliorejeshwa kutoka Marekani, Rais wa Ghana John Mahama alisema Jumatano.
Kuwarudisha watu katika nchi za tatu - mara nyingi maeneo ambayo hawajawahi kuishi - imekuwa sifa kuu ya juhudi za Rais wa Marekani Donald Trump kupambana na wahamiaji wasio na vibali.
Kundi la wahamiaji 14, wakiwemo raia wa Nigeria na Mgambia mmoja, tayari limewasili Ghana, na serikali ilisaidia kuratibu kurejea kwao katika nchi zao za asili, Mahama alisema katika mkutano na waandishi wa habari.
Mahama hakutaja idadi kamili ya wahamiaji ambayo Ghana imekubali kupokea. Pia alitetea uamuzi huo kwa kusema kuwa raia wa Afrika Magharibi 'hawahitaji viza' kuingia Ghana.
Safari bila viza
Rais wa Ghana alisema nchi yake imekubali kupokea raia kutoka Afrika Magharibi, ambapo kuna makubaliano ya kikanda yanayoruhusu safari bila viza.
"Tulikaribishwa na Marekani kupokea raia wa nchi za tatu waliokuwa wakiondolewa Marekani. Na tulikubaliana nao kwamba raia wa Afrika Magharibi walikubalika," Mahama alisema.
Rais Trump analenga kuwafukuza wahamiaji mamilioni walioko Marekani na utawala wake umeongeza juhudi za kuwarejesha watu katika nchi za tatu, ikiwa ni pamoja na kuwatuma wahalifu waliopatikana na hatia kwenda Sudan Kusini na Eswatini, iliyokuwa ikiitwa Swaziland.
Ghana kwa muda mrefu imekuwa makazi ya wahamiaji kutoka Nigeria, ingawa wiki za hivi karibuni zimekuwa na maandamano ya hapa na pale dhidi ya Wanigeria katika miji kadhaa ambapo makundi ya waandamanaji wakitaka raia hao wa kigeni kutimuliwa, kwa madai kuwa wamechangia ongezeko la uhalifu, ukahaba na ushindani usio wa haki wa kiuchumi.
Mwisho wa Julai, Nigeria ilituma mjumbe maalum na Wizara yake ya Mambo ya Nje ilihimiza utulivu huku maafisa wa Ghana na Nigeria wakifanya mazungumzo ya kupunguza mvutano.
Makubaliano ya kurejesha wahamiaji yanakuja wakati Washington imeongeza ushuru kwa bidhaa za Ghana na kupunguza idadi ya viza zinazotolewa kwa raia wake.
‘Kuzidi kuimarika’ kwa mahusiano
Mahama alielezea mahusiano kati ya Accra na Washington kama 'yanayoimarika', ingawa alisema mahusiano hayo yamebaki kuwa mazuri.
Jirani yake Nigeria, kwa upande wake, imekataa kupokea wahamiaji wa nchi za tatu.
"Marekani inashinikiza sana nchi za Afrika kukubali raia wa Venezuela kurejeshwa kutoka Marekani, baadhi yao moja kwa moja kutoka magereza," Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria Yusuf Tuggar alisema katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Channels Television mwezi Julai.
"Itakuwa vigumu kwa Nigeria kukubali wafungwa wa Venezuela," alisema, akiashiria kwamba vitisho vya ushuru wa hivi karibuni vilihusiana na suala la kurejesha wahamiaji.
Katika hatua isiyo ya kawaida, Trump amesimamia kurejeshwa kwa mamia ya watu Panama, wakiwemo baadhi waliorejeshwa kabla ya maombi yao ya hifadhi kushughulikiwa.
Mamia pia wamepelekwa El Salvador, huku utawala wa Marekani ukitumia sheria ya karne ya 18 kuwaondoa watu waliotuhumiwa kuwa wanachama wa magenge ya Venezuela. Baadhi walirejeshwa licha ya majaji wa Marekani kuamuru ndege zilizowabeba zirudi.