MICHEZO
2 dk kusoma
Rudiger wa Real Madrid aomba msamaha kwa kumrushia mwamuzi 'kitu'
Rudiger alikuwa na hasira kutokana na adhabu dhidi ya mchezaji mwenzake Kylian Mbappe katika fainali ya Copa del Rey.
Rudiger wa Real Madrid aomba msamaha kwa kumrushia mwamuzi 'kitu'
Rudiger huenda akakaa nje ya mchezo kwa muda iwapo kamati ya nidhamu itaamua hivyo. / Getty Images
28 Aprili 2025

Mchezaji wa safu ya ulinzi wa Real Madrid Antonio Rudiger ameomba radhi kwa kumrushia mwamuzi kitu jambo lililosababisha kuoneshwa kadi nyekundu wakati wa fainali ya Copa del Rey ambapo walifungwa na Barcelona Jumamosi.

Rudiger, pamoja na mchezaji mwenzake Lucas Vazquez, walionesha hasira baada ya adhabu dhidi ya mchezaji mwenzao Kylian Mbappe katika mechi waliopoteza 3-2.

Refa Ricardo de Burgos Bengoetxea alieleza kuhusu kumuonesha Rudiger kadi nyekundu kwenye ripoti yake, akisema kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32, alitimuliwa uwanjani kutokana na "kurusha kitu akiwa katika benchi, ambacho kitu hicho kilimkosa."

Taarifa zinaonesha kitu ambacho Rudiger alirusha ilikuwa donge la barafu.

Kupitia mtandao wa Instagram, Rudiger, mchezaji wa kimataifa wa Ujerumani, alizungumzia kuhusu tukio hilo. "Hakuna sababu ya mimi kufanya vile," aliweka kwenye mtandao. "Naomba radhi kwa hilo. Naomba msamaha kwa mwamuzi na kwa yeyote ambaye nimemkwaza."

Mchezaji wao mwingine kiungo Jude Bellingham, 21, pia alioneshwa kadi nyekundu.

Kuna wasiwasi kuwa Rudiger huenda akapewa adhabu ya kutocheza mechi kadhaa. Kulingana na kanuni za nidhamu za Shirikisho la Soka la Uhispania (RFEF), kama aliyoyafanya yatasemekana kuwa "vurugu za kadri" kwa mwamuzi chini ya kifungu cha 101, anaweza kupewa adhabu ya kutocheza mechi kati nne na 12.

Iwapo RFEF itaamua kuwa aliyoyafanya ni vurugu zaidi, chini ya kifungu cha 104, ambacho kinazingatia "kumshambulia refa", anaweza kukaa nje ya mchezo kwa kati ya miezi mitatu hadi sita "kama tukio lenyewe lilikuwa moja na halikusababisha hatari yoyote."

Zaidi ya hayo, kama tukio lenyewe litasemekana kuwa "hatari sana" hata kama mwamuzi hakuhitaji kupatiwa matibabu, anaweza akakaa nje ya mchezo kwa kati ya miezi sita na mwaka mmoja.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us