UTURUKI
2 dk kusoma
Waziri wa Uturuki wa Sheria Yilmaz Tunc atetea mahakama huku uchunguzi ukiendelea Istanbul
Yilmaz Tunc amekataa madai ya kuhusishwa na siasa hatua zilizochukuliwa dhidi ya Meya wa Istanbul Ekrem Imamoglu na wengine, akisisitiza uhuru wa mahakama ya Uturuki na kutaka jumuia ya kimataifa kuheshimu mchakato wa sheria
Waziri wa Uturuki wa Sheria Yilmaz Tunc atetea mahakama huku uchunguzi ukiendelea Istanbul
Yilmaz Tunc ametaka kuwepo kwa utulivu na kuheshimu mchakato wa sheria ya Uturuki, na kuzitaka nchi za Ulaya kuwa na mtizamo wenye mizania. AA / AA
27 Machi 2025

Waziri wa Sheria wa Uturuki Yilmaz Tunc ameongea na vyombo vya habari vya kimataifa katika Ofisi ya Rais ya Dolmabahce, na kukataa madai kwamba hatua za kisheria za hivi karibuni dhidi ya Meya wa Istanbul Ekrem Imamoglu na wengine zimechochewa kisiasa.

Waziri Tunc amekosoa jitihada za kuonyesha uchunguzi unaoendelea kuwa umechochewa kisiasa, na kuhimiza kwamba mahakama ya Uturuki iko huru.

 “Tangu kuanza kwa uchunguzi, baadhi wamejaribu kuishinikiza mahakama bila hata kujua undani wa kesi, wakijaribu kuifanya kesi hiyo ya kisiasa. Tunakataa matamshi haya yasiyokuwa na msingi,” amesema.

“Katika taifa ambalo linatawaliwa na sheria, tuhuma za uhalifu sharti zielekezwe mahakamani, na sio barabarani.”

Tunc alitoa taarifa zaidi kuhusu kesi mbili zilizoanzishwa na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Istanbul, zinazohusisha jumla ya washukiwa 106, akiwemo Imamoglu.

Moja wapo ya kesi hizo inahusisha watu saba wanaotuhumiwa kusaidia shirika la kigaidi, watatu wakiwa wanashikiliwa na mmoja akiwa chini ya uthibiti wa mahakama.

 Kesi ya pili imejikita katika tuhuma za hongo, ufujaji wa fedha na ukusanyaji wa taarifa kinyume cha sheria.  Kati ya washukiwa 106, 51 wamekamatwa, 41 wamewekwa chini ya uangalizi wa mahakama, na 14 hawajapatikana.

 Waziri amesema, uchunguzi unategemea zaidi ripoti za uhalifu wa kifedha, na matokeo ya mkaguzi, akitupilia mbali madai ya uingiliaji wa kisiasa.

 “Mchakato wa mahakama utapima madai, utetezi, na ushahidi kwa uwazi kabisa, na kuhakikisha kwamba ukweli unadhihirika,” amesema.

 Tunc pia amelaumu mtizamo wa vyombo vya habari vya kimataifa kwa kuelemea upande mmoja.

“Kwa bahati mbaya, baadhi ya kauli kutoka vyombo vya kimataifa zinadharau misingi ya utawala wa sheria. Tunakataa mtizamo huo hasi dhidi ya Uturuki,” amesema na kuongeza kwamba, wanasiasa katika nchi nyingi wamekabiliana na uchunguzi wa mahakama.

 Ametaka watu wawe na subra na kuheshimu mchakato wa sheria ya Uturuki, na kuzitaka nchi za Ulaya kuzingatia mizania.

 “Heshima kwa mfumo wa sheria ya ndani ya nchi ni jambo la msingi. Tunatarajia uwajibikaji wakati tunasubiri matokeo ya uchunguzi.”

CHANZO:AA
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us