AFRIKA
2 dk kusoma
Ugonjwa wa matende waleta hofu mashariki mwa Uganda
Takwimu za sasa zinaonyesha kuwa watu watano kati ya mia moja katika wilaya ya Kapelebyong wanaishi na ugonjwa huo.
Ugonjwa wa matende waleta hofu mashariki mwa Uganda
Matende hufanya miguu na maeneo mengine ya mwili kufura/ Picha: Getty / Getty Images
28 Aprili 2025

Mamlaka za afya nchini Uganda zimeonyesha wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa wa matende, mashariki mwa nchi.

Mtu ambaye ameambukizwa ugonjwa huu huwa na mabuu (funza) kwenye mfumo wake wa damu na anapoumwa na mbu ambao wanauwezo wa kuchukua mabuu haya  ambayo huendelea kukua na kufikia hatua ya kuambukiza mtu mwingine ndani ya mwili wa mbu.

Kwa kawaida mtu aliyeambukizwa ugonjwa huu huwa na mabuu kwenye mfumo wa damu mwilini mwake wanaojulikana kama microfilariae.

Takwimu za sasa zinaonyesha kuwa watu watano kati ya mia moja wanaishi na ugonjwa huo katika wilaya ya Kapelebyong.

Kwa sasa wakazi 646 wana ugonjwa huu wa matende, hii ni kama asilimia 5.2 ya wakazi wa wilaya hii,” James Eudu afisa wa wilaya wa afya ameelezea.

“Eneo hili lina wakazi 112,500 , hivyo hii ni changamoto kubwa,” Eudu anaongezea.

Maafisa wa afya wanasema maambukizi hayo yamezuia maendeleo, kwani watu walioathiriwa hutumia wakati na pesa kutafuta matibabu na hawawezi kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Tiba ya matende

Mabuu haya husafiri kutoka kwenye mfumo wa damu hadi kwenye mfumo mwingine unaojulikana kama mfumo wa limfu na kuwa minyoo kamili ambayo huziba mfumo huu wa limfu ambao unategemewa sana katika kuweka uwiano sawa wa maji kati ya mfumo wa damu na tishu ndani ya mwili.

Minyoo hii huishi kwa miaka minne hadi sita na katika uhai wake huzaa mamilioni ya mabuu mengine wakati ikiwa kwenye mfumo wa damu.

Wizara ya afya inawashawishi wakazi wa eneo hili kupata tiba mara tu wanaposhuku kuwa na matende.

Dalilli za ugonjwa huu ni pamoja na homa, maumivu ya kichwa, maumivu kwenye jointi na mifupa, kutapika, vidonda kwenye mikono au miguu, mistari ya rangi nyekundu inayoonekana kwenye mikono au miguu.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani, WHO zinaonyesha kuwa matende hutokea katika nchi 39 barani Afrika.

Inakadiriwa kuwa watu milioni 420 wako katika hatari ya ugonjwa huo katika bara, ikiwakilisha 38% ya mzigo wa ulimwengu.

Tiba ya ugonjwa wa matende hutegemea na sehemu husika.

Kwa wagonjwa walio katika jangwa la sahara, tiba ni dawa aina ya albendazole pamoja na ivermectin. Kwa wagonjwa waliopo sehemu nyingine duniani tiba huusisha matumizi ya albendazole pamoja na diethylcarbamazine.

Kwa wale waliovimba korodani kutokana na ugonjwa wa matende, tiba yake ni upasuaji.

Wakati mwingine, kama mgonjwa atakuwa amevimba sana, basi baada ya kufanyiwa  upasuaji wa kawaida, atahitaji kufanyiwa upasuaji kurekebishwa ngozi yake.


CHANZO:TRT Afrika and agencies
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us