Rwanda imezindua mkakati mpya wa kudhibiti ugonjwa wa Malaria katika kukabiliana na ongezeko la maambukizi.
Takriban maambukizi 87,000 yaliripotiwa mwezi Machi pekee na huku mengine 800,000 yakirikodiwa kote nchini mnamo 2024, kulingana na maafisa ya afya ya nchi hiyo.
Mbinu hiyo, inayojulikana kama utambuzi wa kesi tendaji, inatekelezwa na Kituo cha Matibabu cha Rwanda (RBC) katika sekta zilizo na changamoto kubwa ya malaria.
Inahusisha kupima familia yote baada ya mtu mmoja kugundulika kuwa na ugonjwa huo ili kutambua na kutibu wengine ambao wanaweza kuambukizwa lakini bado hawana dalili.
"Mtu anapogundulika kuwa na malaria katika jamii au kituo cha afya, tunafuatilia kwa kuwatembelea nyumbani kwake na kupima kila mtu anayeishi naye," alisema Dkt. Aimable Mbituyumuremyi, Meneja wa Idara ya Malaria na Magonjwa ya Tropiki yaliyosahaulika kutoka RBC.
Lengo ni kugundua maambukizi mapema na kumaliza maambukizi ndani ya familia.
Wizara ya Afya inasema nchini kote, nusu ya wilaya zilichangia asilimia 85 ya maambukizi yote vya malaria yaliyorekodiwa mwezi Machi.
Wilaya ya Gasabo ilirekodi zaidi ya wagonjwa 13,000 wa malaria, idadi kubwa zaidi ya wilaya yoyote. Inafuatwa na Gisagara yenye maambukizi 11,000 na Kicukiro 9,000.
Changamoto nyingine ni kuongezeka kwa upinzani dhidi ya matibabu ya kawaida ya malaria, hasa dawa aina ya Artemether-Lumefantrine (Coartem).
Mnamo Januari, RBC ilianzisha njia mbili za ziada za matibabu Dihydroartemisinin-piperaquine (DHAP) na artesunate-pyronaridine (ASPY).
"Dawa hizi mpya zilianza kutumika Januari. Hazikusudiwi kuchukua nafasi ya Coartem lakini zitumike wakati matibabu ya kwanza yatashindikana," alisema Dkt. Mbituyumuremyi.