Serikali ya Kenya imewataka Wakenya kuhakikisha wanakuwa salama wakati mkondo wa tatu wa Mbio za Dunia za 2025 (WRC), Safari Rally, zikianza.
“Tutatumia ari hii ya mbio za magari katika nchi yetu na ukanda huu kukuza utalii wa michezo. Hii itaongeza idadi ya wageni, kuleta ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi,” amesema Rais Ruto wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo jijini Nairobi.
Mashindano hayo ya kimataifa yatafanyika kuanzia Machi 20 hadi 23 katika mji wa Naivasha ulio na Ziwa wa Naivasha, kilomita 90 kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Nairobi.
Rais Ruto amesema gharama za kuandaa michezo hiyo zimepungua kiasi.
“Mnamo 2023, WRC Safari Rally iligharimu serikali ya Kenya zaidi ya dola milioni 16.2 (Shilingi 2.1 bilioni). Niliagiza Wizara kupunguza kiwango hicho, na kuifanya iwe chini ya zaidi ya dola milioni 10 (shilingi bilioni1.3) mwaka wa 2024. Nina furaha kwamba mwaka huu, gharama imepungua zaidi hadi dola milioni saba (shilingi milioni 908)," Rais Ruto amesema.
Rais Ruto amesema ni muhimu kwa sekta binafsi kuchukua jukumu la kuandaa mashindano hayo na hapo kuipunguzia serikali gharama.

TRT Global - Mbio za magari maarufu World Rally Championship zimepangwa kufanyika katika mji wa Naivasha kati ya 20 hadi 23 mwezi Machi.
Mwaka huu serikali ya Kenya inaunga mkono baadhi ya madereva wa kike.
"Hao ndio wanamitindo halisi na wanaowatia moyo wanawake wajao wa Kenya kukumbatia mchezo huu,” Mvurya amesema.
"Mashindano haya ni mojawapo ya taaluma muhimu ambayo inakuza vipaji katika nchi yetu na serikali inafurahi kuwekeza katika mchezo," Mvurya alisema.
Wataalamu wanasema mwaka huu mashindano yatakuwa na changamoto zaidi.
"Nadhani huu utakuwa mwendo mgumu zaidi kuwahi kuonekana nchini Kenya, ukiendana na uzoefu uliorekodiwa kwenye sehemu ya safu ya Jumatano wakati wa mazoezi," amesema afisa Mkuu Mtendaji wa WRC Safari Rally Kenya, Charles Gacheru
"Madereva wanapaswa kujiandaa vyema kukabiliana na kituo kinachoitwa Camp Moran cha kilomita 32 ambacho naamini kitatenganisha wanaume na wavulana," Gacheru ameongezea.