Ufugaji nzi chuma ulivyogeuka lulu kwa Angela Mauto
Ufugaji nzi chuma ulivyogeuka lulu kwa Angela Mauto
Wakijulikana kama Hermetia Illucens kwa lugha ya kisayansi, nzi hawa hupatikana katika mabara ya Marekani ya Kusini na Kaskazini, sehemu za Afrika, Ulaya, Asia pamoja na Australia.
28 Aprili 2025

Nchini Tanzania, ufugaji wa Nzi chuma umeanza kujizoelea umaarufu, hasa miongoni mwa wafugaji wadogo na vijana wanaojihusisha na kilimo endelevu.

Mmoja wa wanufaika hao ni Angela Mauto.

“Nilijaribu kufuga mende pamoja na nzi chuma lakini nzi chuma walikuwa wana ufanisi zaidi,’’ anasema Mauto katika mahojiano yake na TRT Afrika.

Wakijulikana kama Hermetia Illucens kwa lugha ya kisayansi, nzi hawa hupatikana katika mabara ya Marekani ya Kusini na Kaskazini, sehemu za Afrika, Ulaya, Asia pamoja na Australia.

Kulingana na taarifa kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (Tafiri), idadi ya wafugaji wa nzi chuma imeongezeka kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi karibuni huku serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali yakitoa mafunzo na vifaa kwa ajili ya kukuza ufugaji huo.

Nzi hawa hawana madhara ya aina yoyote kwa binadamu kwa sababu hawana mfumo wa chakula mwilini mwao wala midomo yenye kuwawezesha kula chakula, kama ilivyo nzi wengine wa majumbani.

Chanzo cha lishe

Nzi chuma wanadaiwa kuleta mapinduzi makubwa kwenye upatikanaji wa chakula cha mifugo.

Hii, ni kwa sababu kuwa wadudu hawa wana uwezo wa kukua kwenye aina yoyote ile ya taka hai, ikitoa kiwango cha juu cha protini cha zaidi ya asilimia 50.

“Mwanzoni nilipata wakati mgumu kuwaaminisha watu kuwa kilikuwa ni chakula kizuri kwa mifugo…waliona kama uchafu tu,” anaeleza Mauto, ambaye pia ni mkazi wa jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania.

Mauto alianza ufugaji wa nzi hao mwaka 2018 kama chanzo cha kujitafutia mbolea.

Hata hivyo, alikuja kugundua faida ya nzi hao, hususani kama chakula cha mifugo, kama vile kuku na nguruwe.

“Kuna wakati nilikuwa nawafuga katika mazingira ninayoishi, wakati mwingine ndani ya nyumba nikiishi nao. Jamii ilikuwa hainielewi na hii ilikuwa kwa sababu siku na eneo la kufugia,’’ anaeleza.

Hatua za ukuaji wa nzi chuma

Kuna hatua kadhaa zinazohusisha ukuaji wa nzi hao.

Kwanza ni hatua ya yai, ikifuatiwa na lava, ambacho ndicho chakula cha mifugo, kisha pupa kabla y akiwa nzi kamili.

Nzi huyo ana uwezo wa kuishi kwa siku tano hadi nane.

Rafiki wa mazingira

Kulingana na Mauto, biashara ya ufugaji nzi chuma ni rafiki mzuri wa mazingira kwani hupunguza zitokanazo na vyakula.

Kulingana na utafiti wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), nzi chuma wana uwezo wa kuzalisha takriban asilimia 50 ya uzito wao kama protini, jambo ambalo ni muhimu kwa uzalishaji wa chakula cha mifugo, hivyo kupunguza utegemezi wa mazao ya kilimo yanayotumika kwa chakula cha mifugo.

Licha ya kuwa ni biashara yenye faida nyingi, bado kuna uelewa mdogo kuhusu biashara hiyo.

“Ugumu katika kuwafuga nzi hawa ni pale wanapovamiwa na sisimizi, inakuwa changamoto, lakini kuna namna ya kuwadhibiti na kuwaondoa katika makazi ya nzi hawa.”

Gharama za mayai

Kulingana na Mauto, kilo moja ya mayai ya nzi hao hufikia gharama ya Dola 16,000 za Kimarekani kwa kilo.

Kulingana na Mauto, kilo moja ya mayai ya nzi hao hufikia gharama ya Dola 16,000 za Kimarekani kwa kilo.

“Ninachokiuza mimi ni wadudu wakavu ambao wameshakushwa, na huwa nauza kuanzia Dola za Kimarekani 4,000, kutegemeana na uzalishaji kwa kipindi hicho,” anasema.

Kama anavyosema mwenyewe, ufugaji wa nzi chuma umemuwezesha Mauto kufundisha vijana mbalimbali ili waweze kujitafutia ajira.

Matarajio ya Mauto ni kufungua chuo cha kufundisha ufugaji huu wa nzi chuma hasa kati ya vijana.

Hadi kufikia sasa, Mauto amefanikiwa kuwafikoia zaidi ya vijana 250.

Anatoa wito kwa wanawake wenzake akiwataka waache kuangalia mazingira na kusikiliza maneno ya watu kwa sababu kwa kusikiliza sauti za watu, huwezi kufanya jambo la maana.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us