Namibia hii leo inamuapisha Rais wake wa kwanza mwanamke Netumbo Nandi-Ndaitwah siku ya Ijumaa baada ya kushinda uchaguzi mwaka 2024 ambao uliongeza miaka 35 ya chama tawala madarakani.
Nandi-Ndaitwah, mwenye umri wa miaka 72, atakuwa mmoja wa viongozi wachache wanawake katika ukanda huo katika hafla iliyohudhuriwa na wakuu wa nchi jirani.
Hapo awali alikuwa makamu wa rais, yeye ni gwiji wa Shirika la Watu wa Afrika Kusini Magharibi (SWAPO) ambalo liliongoza nchi hiyo yenye wakazi wachache na yenye utajiri wa madini ya uranium kupata uhuru kutoka kwa utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini mwaka 1990.
Kuapishwa kwa Rais mpya kunafanyika sambamba na maadhimisho ya uhuru wa Namibia.
Maarufu kwa herufi za mwanzo za majina yake, NNN, Nandi-Ndaitwah alipata 58% ya kura katika uchaguzi wa Novemba uliokumbwa na hali ya wasiwasi baada ya kuongezwa muda kwa mara kadhaa kutokana na ucheleweshaji wa vifaa vya kupigia kura.
Suala muhimu katika uchaguzi huo lilikuwa ukosefu mkubwa wa ajira miongoni mwa vijana, huku 44% ya vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 34 wakiwa bila kazi mwaka 2023 katika nchi yenye watu milioni tatu tu.
Katika mkesha wa kuapishwa kwake, NNN aliahidi kushughulikia ukosefu wa ajira kama kipaombele chake.
"Katika miaka mitano ijayo ni lazima tuzalishe angalau nafasi za kazi 500,000," aliliambia Shirika la Utangazaji la Taifa la Afrika Kusini SABC, akiongeza kwamba itahitaji uwekezaji wa dola bilioni 85 za Namibia (dola bilioni 4.67, euro bilioni 4.3).
Nafasi za kazi
“Sekta muhimu za uzalishaji wa ajira ni kilimo, uvuvi na tasnia ya ubunifu na michezo,” alisema. Aliomba umoja baada ya mgawanyiko wa kisiasa kuibuka wakati wa uchaguzi, ambao IPC ilitaka kuubatilisha katika hatua ya mahakama iliyoshindwa.
"Tunaweza kufanya siasa zetu wakati wa kampeni na kadhalika, lakini mara tu itakapokamilika, lazima tuijenge Namibia pamoja," alisema.
"Tunaweza kufanya siasa zetu wakati wa kampeni na kadhalika, lakini mara tu itakapokamilika, lazima tuijenge Namibia pamoja,"
Juu ya kuchaguliwa kwake kama rais wa kwanza mwanamke wa Namibia, aliiambia SABC: "Bila shaka ni jambo zuri kwamba tunavunja dari; tunavunja kuta."
NNN, binti wa mchungaji wa Kianglikana, amechukua msimamo mkali dhidi ya utoaji mimba, ambao umepigwa marufuku nchini Namibia isipokuwa katika mazingira ya kipekee.
Ndoa ya mashoga pia ni haramu nchini humo.
Mwanachama wa SWAPO tangu ujana wake, alihamishwa huko Moscow wakati wa mapambano ya ukombozi.
Akiwa Waziri wa Mambo ya Nje, kati ya 2012 na 2024, alisifu "uhusiano mzuri wa kihistoria" wa nchi yake na Korea Kaskazini.
Namibia ni nchi ya tatu kwa uzalishaji wa urani asilia duniani.
Nchi hiyo pia ina utajiri mkubwa wa almasi na inatarajia kutumia gesi asilia.
Ina uwezo mkubwa wa kuzalisha nishati ya jua na upepo.