Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameadhimisha Siku ya Ataturk, Vijana na Michezo.
Katika ujumbe uliotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki kupitia mtandao wa X Jumatatu, Erdogan ameonyesha umuhimu wa kihistoria wa Mei 19, ukiashiria mwanzo wa Mapambano ya Uhuru wa Uturuki yaliyoongozwa na Mustafa Kemal Ataturk, mwanzilishi wa Jamhuri ya Uturuki mwaka 1919.
“Tunalinda nchi na Jamhuri-sera tukufu tulizoachiwa na waanzilishi wetu-na tunachukua hatua kuendelea na kuiinua Jamhuri ya Uturuki, ambayo itadumu daima, katika kila nyanja,” amesema rais wa Uturuki.
Erdogan amesisitiza kwamba, anawaona vijana wa Uturuki kwamba sio tu ni wasanifu wa mustakbali, lakini pia ni waleta mageuzi, na kusema kwamba anaamini hilo kutokana na nguvu zao, dhamira, na ndoto- na kubeba mtazamo wa “ustaarabu wetu katika nyoyo zao”-vijana wa Kituruki wataacha alama “katika zama zetu kama ‘Karne ya Uturuki.”
Mustakbali wa Uturuki
Katika kujenga mustakbali wa Uturuki, “tunatatua na kuondoa kabisa” tatizo lolote ambalo litapoteza nguvu za vijana wa Kituruki na rasilimali za nchi kwa “majadiliano yasiyokuwa na tija,” amesema.
“Tunafanya kazi kwa nguvu zetu zote kutimiza ahadi yetu ya kuwaachia vijana amani, teknolojia ya hali ya juu, na nchi iliyoendelea.”
“Tunatoa fursa kwa vijana wetu kutambua uwezo wao katika kila nyanja, kuanzia sayansi mpaka Sanaa, michezo mpaka kilimo, diplomasia mpaka teknolojia ya nuklia, na tunakwenda hatua kwa hatua na vijana wetu kutambua misingi yetu ya kuwa taifa lenye nguvu la Uturuki,” amesema Rais.
Amesema kwamba wataendelea kuwaunga mkono vijana wote wa Uturuki ambao wanapambana kufikia malengo yao, bila kukata tamaa, na wanaotaka kuendeleza urithi wa ustaarabu waliorithi kutoka kwa mababu zao.
Siku ya Watoto na Michezo
Rais wa Uturuki amesema kwamba daima wataendeleza dhamira yao ya kufanya kazi kwa bidii na kufikia malengo zaidi kwa vijana wa Uturuki kwa kutambua kila mafanikio yao ya Uturuki, “ambayo imekuwa nchi muhimu huku ikiwa na nguvu na imejiongezea nafasi yake kwa hatua tulizochukua.”
Erdogan pia amewaenzi “mashujaa wetu wa Vita vya Uhuru, hasa Gazi Mustafa Kemal.”
Mei 19, 1919, ni siku ambayo Ataturk, ambae baadae alikuwa mwanzilishi wa Jamhuri ya Uturuki, aliwasili katika mji wa Samsun ulio katika Bahari Nyeusi akitokea Istanbul kuanzisha mapigano ambayo miaka minne baadae yalibadilisha taifa kuwa Uturuki ya kisasa.
Mwaka 1938, Ataturk aliitenga Mei 19 kwa vijana wa taifa la Uturuki kama Siku ya mapumziko ya Taifa kwa Vijana na Michezo ambapo vijana watashiriki katika michezo na shughuli za kitamaduni huku kukiwa na sherehe rasmi nchi nzima.