Serikali ya Uganda imesimamisha mabasi ya Kampuni inayoitwa YY Coaches kutoa huduma kama njia ya tahadhari.
“Zimesimamishwa kwa siku 15 kwa uratibu wa wizara na Kurugenzi ya Usalama Barabarani ya Polisi Uganda,” Byamukama Fred, Waziri wa Nchi wa Usafiri Uganda amesema katika taarifa.
Mabasi hayo yanatoa huduma ya kusafirisha abiria Mashariki na Kaskazini Mashariki mwa Uganda.
“Wameazimia kusitisha shughuli za mabasi ya kampuni ya YY kufuatia msururu wa ajali mbaya zinazohusishwa na uendeshaji wa kizembe,” Waziri ameongezea.
Kampuni hiyo imeshutumiwa kwa madereva wake kuendesha gari kwa uzembe na usimamizi mbaya uliosababisha ajali kadhaa.
Katika wiki mbili mabasi haya yameripotiwa kufanya ajali mara mbili, ya hivi karibuni ilikuwa Mei 5 iliyoua abiria watatu.
Katika ajali moja dereva aliripotiwa kuwa alikuwa akiendesha kwa kasi mno, huku akijaribu kukwepa bodaboda barabarani lakini akashindwa kulidhibiti gari na hatimae likapenduka na kuungua na kufanya hasara kubwa.
Mmoja kati ya abiria bado hajulikani alipo licha ya vyeti na mizigo yake kutambulika.
Masharti mapya
Wakati wa Kusimamishwa huku, Wizara ya Usafiri imesema mamlaka hiyo itafanya ukaguzi wa beji na vibali vya udereva, ratiba za madereva na historia yao ya mafunzo.
Pia mamlaka husika itafanya uchunguzi wa matumizi ya madereva wenye umri mkubwa, na wasio na sifa.
Waziri wa Nchi wa Usafiri amesema uendeshaji wa mabasi unaweza kuanza tena baada ya ukaguzi kukamilika.
Katika wiki mbili mabasi haya yameripotiwa kufanya ajali mbili, kwa mafano ile iliyotokea katika katika barabara ya Katusi na kusababisha vifo kadhaa.