AFRIKA
2 dk kusoma
Moshi mweusi Vatican mchakato wa kura siku ya kwanza wakamilika
Papa mpya hakuchaguliwa baada ya kura ya kwanza kupigwa kwa lengo la kumchagua kiongozi huyo wa 267 wa Kanisa Katoliki duniani.
Moshi mweusi Vatican mchakato wa kura siku ya kwanza wakamilika
Moshi mweusi ukionekana kutoka Kanisa la Sistine Vatican. / Vatican News
7 Mei 2025

Moshi mweusi ulionekana kutoka kwenye bomba la Kanisa la Sistine saa tatu usiku siku ya Jumatano, ishara kuwa kura ya kwanza imepigwa na kukamilika lakini Papa mpya hajachaguliwa.

Watu karibu 45,000 walikuwa wamekusanyika katika Medani ya Mtakatifu Peter kusubiri tangazo hilo ambalo kwanza lilitarajiwa saa moja usiku. Walilazimika kusubiri hadi saa tatu usiku na ndipo moshi mweusi ukaonekana.

Wakiendeleza utamaduni wa miongo mingi, makadinali 133 walikusanyika Vatican kuanza mchakato wa kumchagua Papa wa 267 kiongozi wa Kanisa Katoliki, kufuatia kifo cha Papa Francis mwezi uliopita.

Siku ilianza kwa misa maalum katika Kanisa la Mtakatifu Peter, ikiongozwa na Kadinali Giovanni Battista Re, ambaye pia aliongoza misa ya kipindi cha uchaguzi wa Papa Francis mwaka 2013.

Baadaye, makadinali wakakusanyika katika Kanisa la Pauline na kuelekea katika Kanisa la Sistine, ambapo uchaguzi unafanyika.

Milango ya Kanisa la Sistine, itafungwa hadi pale Papa mpya atakapochaguliwa.

Sheria za uchaguzi huo, ni thuluthi mbili ya wingi wa kura ili kumpata kiongozi mpya.

Uchaguzi huu unaendeleza utamaduni ulioanza 1492, wakati uchaguzi wa kwanza wa kumchagua Papa ulipofanyika katika Kanisa la Sistine — ni mwaka huohuo ambapo Christopher Columbus alifika maeneo ya Amerika.

Pamoja na kuwa mchakato wa kumchagua Papa wakati mmoja uliendelea kwa miaka kadhaa, katika miaka ya kati ya 1200, miaka ya hivi karibuni uchaguzi huo umekuwa wa haraka.

Mwaka 2013, Papa Francis alichaguliwa baada ya upigaji kura mara tano katika kipindi cha zaidi ya siku mbili.

Papa Francis alifariki dunia 21 Aprili akiwa na umri wa miaka 88, kutokana na kuugua ikiwemo mshtuko wa moyo.

Upigaji kura utaendelea tena siku ya Alhamisi wakati Kanisa Katoliki likisubiri kiongozi wao mpya.

Iwapo Papa mpya atachaguliwa, moshi mweupe utaonekana kutoka kwenye bomba na maneno "habemus papam" (Kilatini ikiwa na maana "tumempata Papa") yatatamkwa na kadinali mwandamizi kutoka kwenye roshani ya Kanisa la Mtakatifu Peter.

CHANZO:AA
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us