Takwimu za seriklai ya Rwanda zinaonesha kuwa nchi hiyo ina wakunga wapatao 2,200.
Ripoti ya Taasisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Rwanda inaonesha kuwa wakunga hawa wamesaidia kina mama kujifungua watoto 341,000 wakiwa salama mwaka 2024.
Wizara ya afya inakadiria kuwa nchi itahitaji zaidi ya mara mbili ya idadi hiyo ifikapo mwaka 2028.
"Tunapopungukiwa na wafanyakazi, ni vigumu kuwa na wakati wa kutosha wa kumhudumia kila mwanamke wakati wa kujifungua au kutoa usaidizi wa kunyonyesha. Hii inaweza kuathiri afya ya mama, na hatimaye, hatua ya kujifungua kwa jumla," Dkt. Josephine Murekezi Rais wa Chama cha Wakunga cha Rwanda alisema.
"Mara nyingi wanapokuwa kwenye zamu, wakunga hujikuta wakihudumia wagonjwa wengi zaidi kuliko kawaida, hii ikimaanisha kufanya kazi kwa muda mrefu, na kupata muda mchache wa kupumzika, na kujikuta katika mazingira yenye shinikizo kila wakati,” aliambia vyombo vya habari nchini Rwanda.
Dkt. Menelas Nkeshimana, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya afya, katika Wizara ya Afya, anasema kuna wakunga 2,236 pekee waliosajiliwa na kupewa leseni kote nchini kufikia Machi mwaka huu.
Makadirio ya mpango wa serikali unaotaka kuongeza mara nne ya idadi ya wafanyakazi wa afya wa Rwanda, yanaonesha kuwa katika miaka minne zaidi ya wakunga wapya 5,000 wanatarajiwa kujiunga na idara hiyo.
"Kwa kweli, kila mwanamke aliye wakati wa kujifungua anatakiwa kusaidiwa na wakunga wawili," Dkt. Nkeshimana alisema.
"Lakini ukweli ni tofauti, mkunga mmoja anaweza kujikuta akihudumia zaidi ya wanawake 10 kwa wakati mmoja. Wana kazi kubwa."