Mwanaharakati wa upinzani nchini Uganda aliyetoweka ambaye mtoto wa Rais alidai kumshikilia katika chumba chake cha chini ya ardhi alifikishwa mahakamani akiwa anachechemea siku ya Jumatatu, na kushtakiwa kwa wizi na kurudishwa gerezani, kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine na wakili wake walisema.
Eddie Mutwe, ambaye jina lake halisi ni Edward Ssebuufu, na ambaye pia ni mlinzi mkuu wa Bobi Wine, alitoweka Aprili 27 baada ya kunyakuliwa karibu na mji mkuu wa Kampala na watu wenye silaha, kulingana na chama chake cha National Unity Platform.
Katika msururu wa machapisho kwenye mtandao wa X wiki jana, Muhoozi Kainerugaba, Mkuu wa Jeshi la Uganda na mtoto wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, alisema alimkamata Mutwe "kama panzi," na alimweka chumbani kwake na kutishia kumnyanyasa.
Kainerugaba anaonekana sana kuwa anaandaliwa kumrithi babake mwenye umri wa miaka 80 ambaye ametawala Uganda tangu 1986.
Katika video iliyochapishwa na gazeti ya nchini humo Daily Monitor, wakili wa Mutwe, Magellan Kazibwe alisema mteja wake amefikishwa katika mahakama ya hakimu mkuu mjini Masaka, kilomita 140 (maili 87) kusini mwa mji mkuu wa Kampala na kushtakiwa kwa wizi wa kawaida na wizi wa kuchokoza.
“Yeye (Mutwe) amenieleza mimi na mwenzangu kuwa alikuwa akiteswa kila siku... walikuwa wakimkata na umeme,” Kazibwe alisema.
"Ana maumivu makali, amekuwa hapati dawa, hajamuona daktari yeyote."
Waziri wa Sheria wa Uganda amekashifu hali ya Eddie Mutwe.
“Hakuna raia anayepaswa kuadhibiwa isipokuwa atakapopatikana na hatia baada ya taratibu zinazostahili kuchukuliwa mahakamani,” alisema katika taarifa yake Nobert Mao, Waziri wa Sheria wa Uganda.
“Kuwaleta washukiwa waliokamatwa kikatili na kuteswa kinyume cha sheria mbele ya mahakama ni kukosa heshima kwa michakato ya sheria na unaambatana na unyanyasaji wa haki za kikatiba za washukiwa,” Mao aliongezea.
Eddie Mutwe, alirudishwa gerezani baada ya kushtakiwa. Bobi Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, alisema katika chapisho kwenye X.
Siku ya Ijumaa Tume ya Haki za Kibinadamu ya Uganda, chombo cha serikali, iliamuru Kainerugaba kumwachilia Mutwe, ambaye walisema alikuwa amezuiliwa kinyume cha sheria.