Mwendo wa saa sita na nusu mchana saa za Afrika Mashariki, moshi mweusi ulionekana katika paa la Kanisa la Sistine, Vatican, kuashiria kuwa bado makadinali hawajampata Papa mpya.
Hii inaamanisha kuwa, makadinali 133 waliofungiwa ndani ya Kanisa hilo hawajafikia theluthi mbili ya kura kwa mgombea yeyote.
Alhamisi ni siku ya pili ya upigaji kura katika mkutano huo, ambao ulianza alasiri ya Mei 7 na duru ya kwanza ya upigaji kura ambayo pia ilitoa moshi mweusi.
Maelfu ya waumini wamekusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, wakitarajia kushuhudia historia.
Makadinali hao watapiga kura mara nne kila siku: mara mbili asubuhi na mara mbili alasiri.
Ikiwa papa mpya hatachaguliwa kwenye kura ya asubuhi ya kwanza, kura ya pili inafanyika mara moja.
Kura zote mbili huchomwa pamoja, na kutoa moshi kama uliyoonekana mchana wa leo.
Utaratibu huo unarudiwa mchana.
Baada ya mapumziko mafupi, kura mbili zaidi zitafanyika.
Ikiwa hakuna hata mmoja, moshi unatarajiwa mara mbili za jioni.
Hata hivyo, ikiwa papa angechaguliwa katika kura ya kwanza ya alasiri, moshi mweupe ungeonekana muda mfupi baada ya saa kumi na moja na nusu jioni.
Hivyo, siku zote mbili za Alhamisi na Ijumaa, watazamaji wanapaswa kuwa macho kwa nyakati nne zinazowezekana wakati moshi unaweza kutokea kila siku: mara mbili karibu na saa sita mchana na mara mbili jioni.
Makadinali hao wanafuata utaratibu uliopangwa wakati wa kongamano hilo, linaloanza kila siku kwa Misa, halafu kupiga kura.