Uturuki imekuwa nchi ambayo dunia inaitizama kama mdau mkuu katika diplomasia ya amani, misaada kwa dunia, na upatanishi, rais wa nchi hiyo amesema.
"Mapema, tulizungumza na Rais wa Ukraine (Volodymyr) Zelensky. Wiki iliopita, pia tulijadiliana hili suala la (Ukraine) na Rais Trump, tukizungumzia kuhusu hatua ambazo tutachukua kumaliza umwagikaji damu,” Recep Tayyip Erdogan amesema baada ya kuongoza kikao cha baraza la mawaziri katika mji mkuu Ankara siku ya Jumatatu.
“Pia tunamuunga mkono rafiki yangu mpwendwa (Rais wa Marekani Donald) Trump kwa utashi wake wa kutaka kumaliza mapigano kwa njia ya mazungumzo na diplomasia. Ashukuriwe Mungu, Uturuki imekuwa nchi ambayo watu wanaihitaji kwa kutoa misaada, kuunga mkono jitihada, na upatanishi katika diplomasia ya amani duniani .”
Kuhusu juhudi zinazoendelea za kumaliza vita vya Urusi na Ukraine, ambavyo vinaingia mwaka wake wa nne sasa, Erdogan anasema kuwa “kama nchi pekee inayoaminiwa na pande zote mbili,” Uturuki iko tayari kutoa mchango wake katika mazungumzo ya Alhamisi ya amani kati ya Urusi na Ukraine jijini Istanbul na tunafuraha kuwa wenyeji wa mazungumzo hayo.
Mawasiliano ya hivi karibuni kwa Urusi na Ukraine yameleta fursa mpya, anasema Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, akiongeza kuwa anaamini fursa hii ‘haitopotezwa’
Kuhusu uhasama kati ya Pakistan na India, Erdogan alieleza kufurahishwa kwake na hatua ya kusitishwa kwa mapigano kati ya mataifa hayo mawili, na kutoa wito kwa pande zote mbili kujiepusha na uchokozi katika siku za baadaye.
Kuhusu kutangazwa kusambaratika kwa kundi la kigaidi la PKK na kusalimisha silaha, Erdogan anasema hii ni hatua muhimu katika suala la usalama wa taifa la Uturuki, katika kanda, na kupatikana kwa amani ya kudumu katika nchi.
“Tunaamini kuwa tangazo la PKK kusambaratika ni uamuzi unaojumuisha matawi yake yote, hasa Iraq kaskazini, Syria, na Ulaya,” aliongeza.