Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu masuala ya amani nchini Libya (UNSMIL) imetangaza kuundwa kwa “kamati ya amani” kwa kushirikiana na Baraza la Rais Libya kufuatia mapigano ya hivi karibuni katika mji mkuu wa Tripoli.
Katika taarifa ya Jumapili, UNSMIL imesema kuwa hali ya makubaliano ya usitishaji wa mapigano ya Mei 14 bado ni tete, na kuhimiza kamati kujikita katika kuhakikisha kudumu kwa amani na kulinda raia.
Kamati, imefanya mkutano wake wa kwanza ambao mwenyekiti wake ni Mkuu wa Majeshi, Mohamed Al-Haddad.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Baraza la Rais, mkuu wa baraza, Mohamed al-Menfi, amekutana na Hanna Tetteh, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu kwa Libya na kiongozi wa UNSMIL, Haddad na wakuu wa jeshi wa vikosi maalumu wa Libya kutathmini maendeleo ya hivi karibuni jijini Tripoli.
Mapigano yaliibuka Jumatatu ya Mei 14 mjini Tripoli kufuatia kifo cha Abdel Ghani al-Kikli, ambae alikuwa kiongozi anayesimamia masuala ya kuleta utulivu.
‘Ufanisi wa jeshi, polisi’
Muda mfupi baada ya kifo cha al-Kikli, serikali ilitangaza kwamba brigedia nambari 444, kutoka Wizara ya Ulinzi, imeshikilia makao makuu ya ofisi inayosimamia utulivu jirani na Abu Salim na kudhibiti eneo hilo.
Katika taarifa ya wiki iliyopita, Waziri Mkuu wa Libya Abdul Hamid Dbeibeh alilipongeza jeshi na polisi kwa ufanisi wao wa kudhibiti hali baada ya yaliyojiri katika mji huo.
Mapigano yalianza mapema Mei 14 katika eneo la Rada, ambalo linafahamika kwa kuwa na vikosi vya wapiganaji wenye nguvu mjini Tripoli, vikosi vya serikali, huku moshi ukionekana katika baadhi ya majengo.
Wizara ya Ulinzi baadae siku hiyo ilitangaza kuwepo kwa usitishaji wa mapigano katika maeneo yote ya Tripoli kama sehemu ya jitihada za kulinda raia.
Afisa mmoja wa masuala ya Afya katika manispaa ya Tripoli, Mohamed Abedl Wahab, ametanga kuuawa kwa watu sita na wengine 70 kujeruhiwa katika mapigano hayo.