Safari ya Judith Jebet katika ufugaji nyuki na urinaji asali
Safari ya Judith Jebet katika ufugaji nyuki na urinaji asali
Mara baada ya kumaliza elimu ya juu, Judith Jebet alikuwa na ndoto za kuwa mwandishi wa habari.
24 Mei 2025

Judith Jebet anajaza asali kwenye glasi, huku wasaidizi wake wakizungushia vitambaa, na kuvisha nembo ya kampuni yake ‘Soin Honey’, na kuiweka kwenye mifuko tofauti.

Kwa sasa, Jebet ana mkataba wa kusambaza mikebe 300 ya asali katika kampuni ambayo inataka kuwazawadia wafanyakazi wake.

“ Nilianza kwa kuuza asali kama mzaha tu kwani rafiki yangu alikuwa anauza. Nikaanza na kununua lita tano kutoka kwa wakulima vijijini, ninapakia kwa mikebe ya plastiki na kuuza kwa marafiki. Ndipo nilipokuja kugundua kuwa kuna soko kubwa la biashara hiyo,” anasema Jebet katika mahojiano yake na TRT Afrika.

Mara baada ya kumaliza elimu ya juu, Judith Jebet alikuwa na ndoto za kuwa mwandishi wa habari.

Waswahili wanasema; usilolijua, ni kama usuku wa giza. Na ndivyo ilivyokuwa kwa Mkenya huyo, hakufahamu kuwa biashara ya asali, na sio uandishi wa habari, ndiye iliyokuwa ikimngojea.

Jebet anatokea katika eneo la Baringo, ambapo wazalishaji asali huvuna asali ya asili kwa viwango vidogo vidogo.

Kutoka kwenye mzinga hadi mezani

Kulingana na Jebet, idadi ya wazalishaji asali katika eneo la Baringo ilizidi kupungua, kwani walikata tamaa kutokana na mapato duni kutoka kwa mauzo ya asali zao.

Kama anavyosema mwenyewe, hali hii ilichangiwa kwa kiasi kikubwa na wazalishaji hao kuzalisha vidogo vya asali na kutumia mbinu zisizo za kisasa, na zenye kuchosha.

“Niliamua kufanya uzalishaji wote kutoka kwenye mizinga hadi mezani,” anaieleza TRT Afrika.

“Niliona kuwa ningeweza kuvuna asali kwa wingi, yenye ubora na ikanipatia mapato.”

Baada ya kushauriana na wazazi wake, Jebet alipewa shamba katika eneo la bonde la Kerio, katika katika kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Bonde la Kerio liko kati ya Milima ya Tugen na miinuko ya Elgeyo kwenye mwinuko wa mita 1,000, katika Bonde Kuu la Ufa nchini Kenya.

Mto Kerio unapita kwenye bonde hili, na hivyo kutengeneza mazingira mazuri na ya kipekee.

Hali ya hewa katika Bonde la Kerio hutawaliwa joto pamoja na ukavu, na mvua za hapa na pale, ukilinganisha na maeneo mengine ya Kenya.

Hali hii, hutengeneza mazingira sahihi kwa kufunga nyuki wa asali.

Subira huvuta heri

Shamba la Jebet, ambalo lina miti mingi, linapatikana katika eneo lenye watu wachache, na hivyo kulifanya liwe eneo sahihi kwa ufugaji nyuki na urinaji asali.

Mwishoni mwa mwaka 2021, Jebet alianza safari ambayo ilimfunza umuhimu wa subira.

“Nilianza na mizinga 50 ya nyuki. Itakuchukua muda ili uanze kurina asali, kwani ni lazima nyuki waingie kwenye mizinga na kuanza uzalishaji wa asali.”

Kwa sasa, Jebet ana mpango wa kuanza mizinga mingine 50.

“Unaweza kuwa na ardhi, lakini hilo halimaanishi kuwa utaweza kuweka mizinga ya nyuki hapo kwa sababu nyuki wana tabia ya kuhama, wakikwepa uwepo na usumbufu kutoka kwa binadamu,” anasema Jebet.

Jebet amejipa kipindi cha miaka mitano ili aanze kuzalisha asali ya kutosha kwa mahitaji ya soko la ndani.

Anawakumbuka wazalishaji wengine

Licha ya kuendeleza miradi yake mwenyewe, Jebet hajawasahau wazalishaji wenzake alioanza nao safari ya ufugaji nyuki katika eneo lake.

“Wakulima wadogo wadogo wa asali ni muhumi sana kwangu, wanachangia kama asilimia 70 ya asali ambayo kampuni yangu ya Soin Honey inauza kwa sasa. Kampuni bado ni changa kwa hivyo hatuwezi kutosheleza soko kutoka kwa mizinga yetu pekee kwa sasa.”

Mpango wake ni kuwaleta karibu wakulima hao na kuwapa mafunzo ya kuzalisha asali, kwa kutumia mbinu za kisasa ili wazalishe zaidi na kupata mapato makubwa.

“Nina wakulima ambao nimekuwa mteja wao katika maeneo ya Baringo, Pokot Magharibi, hadi maeneo ya mpakani na Uganda kwa hivyo lazima pia tuwasaidie wazalishe kwa njia za kisasa ili sisi tukipungukiwa kutoka upande huu wa Kerio Valley tunapata asali yenye ubora kama wetu kutoka kwao.”

Kazi ndiyo imeanza

Kwa sasa, kampuni ya Jebet ya Soin Honey imesajiliwa na serikali na kupewa chapa ya ubora, na kazi sasa ni kwake kutumia mitandao ya kijamii, maonesho tofauti nchini na mapendekezo kutoka mnunuzi mmoja hadi mwingine kunadi asali yake.

Kila mwezi, Jebet ana uhakika wa kuuza takribani kilo 500 za asali, huku kilo moja ikiuzw akwa Dola 12 za Kimarekani, japo analenga kuongeza kiwango hichi, pindi mizinga yake 100 itakapokuwa tayari.

“ Muonekano wa bidhaa ndiyo kivutio kikubwa cha mauzo ndio maana nimewekeza kwenye chupa na vifungashio salama kwa sababu najua ni uzuri ambao mtu huona nje unamvutia kununua asali yangu ya Soin,” Jebet anaeleza.

Jebet anaangua kicheko anaposema kuwa pamoja na utaalamu wake katika uandishi wa habari, bado angesalia kuuza asali.

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us