Wafahamu wagombea nafasi ya ukurugenzi ndani ya WHO Afrika
AFRIKA
2 dk kusoma
Wafahamu wagombea nafasi ya ukurugenzi ndani ya WHO AfrikaKifo cha Mtanzania, Dkt. Faustine Ndugulile, kililazimu nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, kupendekeza majina mapya ya wagombea ambao watawania nafasi iliyoachwa wazi na mtaalamu huyo wa afya.
Kama ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita, uchaguzi wa Mei 18, utahusisha wagombea wanne, kutoka mataifa manne tofauti./Picha: Wengine
15 Mei 2025

Bara la Afrika linajiandaa na uchaguzi wa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kanda hiyo, mchakato unaotarajiwa kufanyika Mei 18, 2025 jijini Geneva, Uswisi.

Hii inafuatia kifo cha aliyekuwa mkurugenzi mteule wa WHO kwa kanda ya Afrika, Dkt. Dr Faustine Ndugulile kilichotokea mwezi Novemba, 2024.

Dkt. Ndugulile alitarajiwa kuanza majukumu yake mapya ndani ya shirika hilo, mwezi Februari 2025.

Makao makuu ya WHO Afrika, yanapatikana jijini Brazzaville, ndani ya Jamhuri ya Kongo.

Kifo cha Ndugulile, kililazimu nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, kupendekeza majina mapya ya wagombea ambao watawania nafasi iliyoachwa wazi na mtaalamu huyo wa afya kutoka Tanzania.

Hapo awali, Dkt. Ndugulile alichuana na kuwashinda wagombea wengine ambao ni Dkt. Ibrahima Socé Fall wa Senegal, Dkt. Richard Mihigo kutoka Rwanda na Dkt. Boureima Hama Sambo, aliyependekezwa na Niger.

Kama ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita, uchaguzi wa Mei 18, utahusisha wagombea wanne, kutoka mataifa manne tofauti.

Wafuatao ndio wanaowania nafasi ya kumrithi Dkt. Ndugulile ndani ya WHO Afrika na wasifu wao kwa ufupi.

Dkt. Michel Yao, Côte d'Ivoire

Kwa sasa, yeye ndiye mkurugenzi wa programu za dharura ndani ya WHO.

Ni daktari mwenye uzoefu wa zadi ya miaka 27 katika sekta ya afya ya umma.

Katika ahadi zake pindi akichaguliwa kuiongoza WHO Afrika, Dkt. Yao anasema atakuwa tayari kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya afya, hususani kati ya nchi za Afrika na mashirika ya kimataifa.

Dkt. Mohamed Lamine Dramé, Guinea

Ana uzoefu wa muda mrefu katika usimamizi na sekta ya afya ya umma nchini Guinea.

Wakati akijipigia debe nafasi hiyo kwenye mdahalo wa wagombea uliofanyika Aprili 2, 2025, Dramé alisema kuwa analenga kukuza na kuimarisha utayari wa bara la Afrika katika kukabilina na magonjwa ya milipuko.

Profesa Mohamed Yakub Janabi, Tanzania

Kwa sasa ndiye mshauri mkuu wa masuala ya afya wa Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.

Profesa Janabi, ambaye amejizoelea umaarufu kutokana na misimamo yake ya lishe bora na mitindo ya kimaisha yenye kumkinga binadamu na magonjwa yasiyoambukiza, analenga kuongeza ustahimilivu na kulifanya bara la Afrika lijitigemee kwenye sekta ya afya.

Profesa Moustafa Mijiyawa, Togo

Akijulikana sana kwa kuchagiza upatikanaji wa huduma bora ya afya kwa wote, Mijiyawa alikuwa na nafasi muhimu katika kuboresha miondombinu na kuleta maboresho makubwa katika sekta ya afya nchini Togo.

Amelenga kukuza ushirikiano wa kimataifa ndani ya WHO Afrika.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us