Gugumaji jipya linavyotishia uhai wa viumbe hai Ziwa Victoria, Tanzania
AFRIKA
4 dk kusoma
Gugumaji jipya linavyotishia uhai wa viumbe hai Ziwa Victoria, TanzaniaNchini Tanzania Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo aina mpya ya gugumaji lijulikanalo kama ‘Salvinia SPP’ limebainika ndani ya Ziwa Victoria.
Nchini Tanzania, Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo aina mpya ya gugumaji lijulikanalo kama ‘Salvinia SPP’ limebainika katika Ziwa Victoria, ambalo lina uwezo wa kuzaliana zaidi ya mara mbili mpaka tatu kila baada ya siku nane hivyo kufanya ongezeko lake kuwa kubwa ndani ya kipindi kifupi./Picha: TRT Afrika
15 Mei 2025

Samaki na viumbe wengine wa majini wapo hatarini kwenye Ziwa Victoria.

Uwezo wao wa kupumua unazidi kupungua kutokana na uwepo wa aina mpya ya gugumaji katika ziwa hilo, ambalo ni la tatu kwa ukubwa barani Afrika.

“Unaweza ukapeleka maji sehemu ikawa changamoto kwako mwenyewe kwa sababu sisi tuko kibiashara zaidi. Mteja anakuwa hapendezwi na maji uliyompelekea kwani anakuwa hajaridhika kuyatumia,” alisema Sabatho Robert, mkazi wa Kigongo.

Robert, anayejishughulisha na usambazaji wa maji, anasema changamoto kubwa wanayokutana nayo kutokana na magugumaji ni uchafu wa maji kwani upepo unapovuma, maji wanayoyatumia majumbani yanachafuka.

Nchini Tanzania, aina mpya ya gugumaji lijulikanalo kama ‘Salvinia SPP’ limegunduliwa ndani ya Ziwa Victoria Gugu hilo lina uwezo wa kuzaliana zaidi ya mara mbili mpaka tatu, kila baada ya siku nane hivyo kufanya ongezeko lake kuwa kubwa ndani ya kipindi kifupi.

Debora Meleka ni mjasiriamali anayeishi eneo la Kigongo Feri, jijini Mwanza.

Maji machafu

Meleka, ambaye kwa kiasi kikubwa, kipato chake cha kila siku, kinategemea uwepo wa ziwa hilo, magugumaji ni kama yanampa hasara.

“Zamani wakati hakuna magugumaji, maji yalikuwa ni masafi, tulikuwa tunachota hapa hapa, lakini sasa hivi, maji yamekuwa machafu, tunahangaika,” anaeleza.

Hali hiyo, imemfanya Rhoda Francis, mkazi wa wilaya ya Sengerema nchini humo, kuendelea kutumia maji hayo hayo, kwani hawana namna nyingine.

Kuonekana kwa mara ya kwanza

Magugu hayo yalianza kuonekana mwishoni mwa 2024, na wavuvi katika mialo ya Buyagu, Chole, Nyahiti na Mbarika, katika wilaya za Misungwi na Sengerema.

“Kikosi kazi kilibaini aina ya gugumaji, tabia za uzalianaji na usambaaji, mambo yanayosababisha kushamili na maeneo ambayo tayari yameshavamiwa na gugumaji hilo. Pia kikosi kazi kilifanikiwa kuopoa zaidi ya tani 36 za gugumaji katika eneo la Kigongo-Busisi,” anasema Kayombo, katika mahojiano yake na TRT Afrika.

Miezi michache baadaye, ongezeko kubwa la magugu hayo likaanza kushuhudiwa na kuanza kuleta athari mbalimbali kwenye sekta ya uvuvi na vyombo vya usafiri hususani vivuko katika eneo la Kigongo-Busisi, hali iliyozorotesha huduma za usafiri kati ya mkoa wa Mwanza na maeneo mengine yenye kutegemea kivuko hicho.

Katibu wa Vikundi vya Kusimamia Rasilimali za Uvuvi, katika eneo la Kigongo, Deogratius Mashiko anasema kuwa magugumaji yanawapa shida wakati kufanya shughuli zao za uvuvi.

Kulingana na Meneja wa Baraza la Taifa la Usimamizi na Hifadhi ya Mazingira (Nemc) Kanda ya Ziwa Victoria, Jarome Kayombo, wingi wa magugumaji hayo unatokana na ongezeko la virutubisho ndani ya ziwa, jambo linalosababishwa na shughuli za kibinadamu zisizozingatia utunzaji endelevu wa mazingira.

“Kikosi kazi kilibaini aina ya gugumaji, tabia za uzalianaji na usambaaji, mambo yanayosababisha kushamiri kwa magugu hayo. Pia kikosi kazi kilifanikiwa kuopoa magugumaji katika eneo la Kigongo-Busisi,” anasema Kayombo, katika mahojiano yake na TRT Afrika.

Shughuli za kibinadamu

Kasi kubwa ya ongezeko la gugumaji hilo inatokana na shughuli za kilimo, utupaji holela wa taka maji na taka ngumu kutoka viwandani na majumbani, ujenzi wa makazi, shughuli za uvuvi na ufugaji samaki zinazofanyika bila kuzingatia taratibu za utunzaji wa mazingira.

Sababu zingine, ni pamoja na ukataji miti kiholela, na uchimbaji madini bila kuzingatia dhana ya maendeleo endelevu na kuvamia eneo tengefu la mita sitini kutoka kwenye kingo za mito au ziwa.

“Pamoja na kuwepo kwa madhara ya aina mpya ya gugumaji ambayo tayari yameshatukumba, gugumaji hili linaathiri pia maisha ya viumbe hai majini (wakiwemo samaki) kwa kukosa hewa ya oksijeni,” anaeleza mtaalamu huyo kutoka Nemc.

Kulingana na Mkurugenzi wa Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) Dkt. Renatus Shinhu, jumla ya tani 441 za gugu maji aina ya ‘Salvinia Spp’, imeopolewa katika eneo la Kigongo-Busisi mkoani Mwanza, kwa kutumia mitumbwi na zana za kawaida.

“Wakati tunaendelea kusubiri fedha za dharura kutoka Serikali kuu, Wizara ya Maji kupitia Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria imeendelea kuchukua hatua za haraka za kudhibiti ueneaji wa gugumaji hili kwa njia za kawaida kwa kutumia mitumbwi na zana za kawaida kuopoa ili kupunguza athari za gugumaji hasa kwenye eneo la vivuko (Kigongo – Busisi)”, anasema Dkt. Shinhu.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us