Maafisa wa upelelezi nchini Kenya wamemkamata mshukiwa wa mauaji ya mbunge Charles Ong’ondo Were, Kilichotokea Aprili 30, 2025.
Amos Barasa Kasili alikamatwa katika eneo la Kibera Darajani, mjini Nairobi, wakimhusisha na tukio la kupigwa risasi kwa marehemu mbunge wa Kasipul.
Kukamatwa huku kunafuatia uchunguzi wa kina uliounganisha Barasa na washukiwa wakuu na kumuweka katika eneo la uhalifu siku hiyo ya maafa.
Ilibainika kuwa Barasa aliwahi kuwa mwendesha pikipiki ambayo wavamizi hao waliitumia kulifuata gari la mbunge huyo na baadaye pikipiki ya kutoroka baada ya kushambuliwa. Alipokamatwa, Barasa alikutwa akiwa na pikipiki husika.
“Uchunguzi ulibaini kuwa Barasa ni mhalifu aliyezoea kujifanya kama mwendeshaji boda boda, mara nyingi akishirikiana na magenge ya wahalifu wenye silaha wakati wa operesheni zao,” DCI ilisema katika taarifa.
“Wakati wa kuhojiwa, alifichua kuhusika kwake katika uhalifu huo, na kuwa alikuwa alipokea malipo ya Ksh. 50,000 kama sehemu ya fidia yake.
Zaidi ya hayo, pikipiki iliyopatikana kutoka Barasa inalingana na maelezo ya iliyonaswa katika picha za CCTV karibu na Bunge, ambayo ilionekana ikifuata gari la marehemu.
Maelezo ya mshukiwa yalifichua historia yake ya uhalifu, ikiwa ni pamoja na kifungo cha awali katika gereza mjini Nairobi, ambako alikutana na baadhi ya watu waliohusika katika uhalifu huo.
Barasa atafikishwa mahakamani huku uchunguzi ukiendelea.