Kongamano la kwanza la kimataifa la usalama kuhusu Afrika (ISCA) lilianza siku ya Jumatatu katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali, huku Rais Paul Kagame akisema mkutano “ulihitajika kufanyika zamani” na kutoa wito wa kuwepo kwa njia zinazopendekezwa na Waafrika wenyewe kutatua changamoto za kiusalama.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi, Kagame alisema kuwa mustakabali wa Afrika “hautakiwi kuangaziwa na watu wa nje” na kusisitiza kuhusu umuhimu wa bara hilo kuchukua jukumu la kuhakikisha usalama na utulivu wake.
Alisema kuwa kwa muda mrefu usalama wa Afrika umeonekana kama mzigo ambao “unaweza kubebwa na watu wengine,” ikiwa hakuna mchango wa kutosha kutoka kwa bara la Afrika au kuwa na ufahamu ya yanayojiri katika eneo hilo.
“Mtazamo huu haujakuwa na mafanikio na umeshindwa kuleta suluhu kwa bara la Afrika na ulimwenguni,” alisema.
‘Kubadilisha mtazamo’
Kagame aliueleza mkutano huo kuwa na “juhudi za maksudi za kubadilisha mtazamo na pia yanayojiri” wa jukumu la Afrika katika masuala ya usalama duniani.
Alitoa wito kwa mataifa ya Afrika kuchukua jukumu la kuwa washirika wa uhakika katika kutatua masuala ya usalama, akionya kuwa kuachana na jukumu hilo “kunawapa fursa wengine kuingilia, na kupoteza muelekeo na udhibiti.”
Kagame alitoa wito wa kuwepo kwa taasisi zenye uwezo, ikiwemo Umoja wa Afrika na baraza lake la Amani na Usalama, kuliongoza bara liweze kutimiza malengo ya usalama wa pamoja.
“Msingi wa kukabiliana na changamoto za kiusalama upo kwenye uwezo wa kutoa suluhu zetu wenyewe,” alisema, akiongeza kuwa kongamano hilo lazima liende sanjari za utashi wa kisiasa pamoja na utaalamu na maslahi ya taifa kwa bara zima.