Ajali ya Mv Bukoba: Mamlaka za Tanzania zazidi kujipanga, miaka 29 baadaye
AFRIKA
6 dk kusoma
Ajali ya Mv Bukoba: Mamlaka za Tanzania zazidi kujipanga, miaka 29 baadayeMeli ya Mv Bukoba ilizinduliwa mwaka 1979 na Rais wa kwanza wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Julius Kambarage Nyerere, ilidumu kwa miaka 17 tu, na kupinduka ikiwa katika safari zake za kawaida, ikitokea katika bandari ya Bukoba kupitia Kemondo.
Ilizama ikiwa imebakisha umbali wa maili moja na nusu ili iweze kutia nanga katika bandari ya Mwanza Kaskazini, hali ambayo ilikwishawapa abiria matumaini ya kufika salama kwa abiria waliokuwa ndani ya meli hiyo./Picha: Wengine
20 Mei 2025

Miaka 29 iliyopita, Tanzania ilikumbwa na msiba mkubwa kufuatia kuzama kwa meli ya Mv Bukoba.

Tukio hilo lililotokokea Mei 21, 1996, lilisababisha vifo vya watu zaidi ya 800 huku baadhi ya watumishi wa Serikali wakishtakiwa kwa kosa la jinai kutokana na ajali hiyo.

Ikiwa ana abiria kati ya 750 hadi 800, pamoja na wafanyakazi 37, ilizama majini kwenye Ziwa Victoria, katika eneo la mwambao wa Bwiru Jijini Mwanza, takribani kilomita 30 kabla ya kufika nchi kavu.

Tukio hilo, lilitokea nyakati za asubuhi, wakati wengi wa abiria wakiwa wanajiandaa kusafisha vinywa vyao.

Kovu lisilofutika

“Tulikaa miaka mitano bila hata kuwa na kaburi la kuwaombea. Mwili wa mume wangu haukupatikana. Ilikuwa kama kupoteza ndoto zangu zote, ’’anasema Rose Kaswako, mkazi wa eneo la Kirumba jijini Mwanza, ambaye alipoteza mume na watoto wake wawili katika ajali hiyo.

Katika kuhakikisha kuwa tukio kama hilo halijirudii, serikali ya Tanzania ilichukua hatua mbalimbali, za muda mrefu na muda mfupi.

Miongoni mwa hatua hizo, ni pamoja na uundwaji wa kamati ya uchunguzi ambayo ilitoa mapendekezo mbalimbali ya kuimarisha usalama wa usafiri majini.

Mapendekezo

Moja ya mapendekezo hayo ilikuwa ni kuanzishwa kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Majini (SUMATRA), ambayo baadaye ilikuwa kujulikana kama Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), ambacho ndicho chombo chenye dhamana ya kusimamia na kudhibiti usalama wa usafiri majini, Tanzania Bara.

Vile vile, ipo Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO).

Taasisi hiyo imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha mifumo ya meli kutoka analogia kwenda kidigitali ili kuendana na teknolojia ya kisasa.

“Meli zetu zinazingatia mfumo wa kimataifa wa usalama ili kuzuia ajali na kuzuia uharibifu wa mazingira kwenye maji, kama ulivyo utaratibu wa kimataifa chini ya Shirika la Kimataifa la Usafirishaji wa Majini (IMO),” anaeleza Eric Hamissi, Mkurugenzi wa TASHICO.

Kulingana Hamissi, kampuni hiyo imeboresha mifumo ya tiketi mtandao na mageti ya ukaguzi wa tiketi na mizigo ili kuepuka kuzidisha idadi ya abiria wanaiongia kwenye meli.

Ziwa Victoria

Kwa upande wa Ziwa Victoria, TASHICO imeazimia kujenga meli ya kisasa ya mizigo ya tani 3,000 na ujenzi wa kiwanda cha kujenga meli.

“Serikali imekuwa na mipango kadhaa ya kuongeza idadi ya meli na kuboresha huduma za usafiri majini hususani Ziwa Victoria,” anasema.

Hali kadhalika, TASHICO imekuwa ikishiriki kwenye maonesho mbalimbali ya kitaifa katika kuhakikisha inafikisha elimu kwa wananchi yakiwemo Maonesho ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Saba Saba, Siku ya Wakulima maarufu kama Nane Nane, Siku ya Bahari Duniani, Siku ya Mabaharia Duniani na mengine mengi.

 Mikataba ya kimataifa ya usalama

Kwa upande wake, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) linaendelea kutekeleza mikataba ya kimataifa kama ule wa IMO, SOLAS, mikataba ambayo inavitaka vyombo vya usafiri majini kuwa na vifaa vya uokozi ambavyo vinakidhi viwango vya kimataifa.

Ukaguzi wa vifaa hufanyika kwa kila chombo kinaposajiliwa na mara kwa mara, katika kipindi cha robo mwaka.

“Tunashirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) ambayo inaendelea kuimarisha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa mabaharia na meli kwa njia ya kidijitali,” anaeleza Mkurugenzi wa TASAC, Mohamed Salum.

Kulingana na Salum, mfumo huo unalenga kuhudumia meli kwa kuhusisha usajili, ukaguzi, utoaji wa vyeti, ufuatiliaji wa ujenzi na ukarabati wa meli.

“Mfumo huu utarahisisha sana huduma kwa wamiliki wa meli kwa kuwawezesha kupata huduma zote za udhibiti kwa njia moja ya kidijitali,” anaongeza.

Utafutaji na uokozi majini

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa TASAC, serikali imeanzisha Kituo Kikuu cha Kitaifa cha Kuratibu Utafutaji na Uokoaji Majini (MRCC) kilichopo jijini Dar es Salaam.

Kituo hicho kitahusika na upokeaji wa taarifa za ajali kutoka kwa vyombo vya usafiri majini, wananchi au taasisi mbalimbali.

“Kituo hiki hutumia mifumo ya kisasa ya mawasiliano na teknolojia kutambua eneo ambalo ajali imetokea, na kuratibu juhudi za haraka za uokoaji kwa kushirikiana na vikosi vya uokoaji,” anaeleza.

 Ukiukwaji wa Sheria

Licha ya juhudi zinazofanywa na Serikali kupitia taasisi kama TASAC, bado kuna changamoto kadhaa zinazohitaji uboreshaji wa kimkakati. 

Kwa mfano, Sheria na kanuni za usajili wa meli zinakataza meli iliyozidi miaka 15 tangu kujengwa kusajiliwa kwa matumizi ya biashara, lengo likiwa ni kuhakikisha ubora na usalama wa meli.

Hata hivyo, hii inasalia kuwa changamoto kwa wawekezaji wazawa kutokana na gharama kubwa za ununuzi au ujenzi wa meli mpya.

Hali hii imepelekea utegemezi mkubwa kwa meli za serikali na wachache walioweza kumiliki meli ndogo, hali inayopunguza ushindani na ubunifu katika sekta hii.

‘‘Katika baadhi ya maeneo, bado kuna matumizi makubwa ya vyombo vya mbao au magogo ambavyo ni hatari kwa abiria na mazingira. Upatikanaji wa miti ya kutengeneza vyombo hivyo pia unaendelea kupungua. Kuna haja ya kuweka mpango wa kitaifa wa kuwezesha matumizi ya vifaa mbadala na salama zaidi kama ute kioo ndani ya nchini,” anasisitiza Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Uchukuzi nchini Tanzania.

Meli ya Mv Bukoba ilizinduliwa mwaka 1979 na Rais wa kwanza wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Julius Kambarage Nyerere, ilidumu kwa miaka 17 tu, na kupinduka ikiwa katika safari zake za kawaida, ikitokea katika bandari ya Bukoba kupitia Kemondo.

Ilizama ikiwa imebakisha umbali wa maili moja na nusu ili iweze kutia nanga katika bandari ya Mwanza Kaskazini, hali ambayo ilikwishawapa abiria matumaini ya kufika salama kwa abiria waliokuwa ndani ya meli hiyo.

Ilikuwa tayari iko jirani kabisa na ufukwe wa Shule ya Sekondari Bwiru, ambako sasa kumejengwa mnara wa kumbukumbu ya wahanga wa ajali hiyo mbaya kuwahi kutokea katika Ziwa Victoria.

Ukosefu wa vifaa vya kuokolea majini ulikuwa ni chanzo cha kuongezeka kwa vifo vya abiria, waokoaji wa ajali hiyo walisubiriwa kufika nchini kutokea Afrika Kusini, ambao waliweza kuogelea na kuokoa baadhi ya maiti chache zilizokuwa zimezama umbali wa mita 25 chini ya maji.

Ajali hiyo imebaki kuwa kumbukumbu mbaya kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa na mikoa jirani na Watanzania kiujumla. Kila mwaka ifikapo Mei 21, Tanzania hukumbuka kwa kuomboleza vifo vya abiria waliokuwa ndani ya meli hiyo.

Baadhi yao miili yao haikupatikana na kusababisha maziko yao kufanyika humo humo majini huku meli hiyo ikigeuzwa kuwa kaburi lao la pamoja.

Makaburi ya wahanga wengine yapo katika Kitongoji cha Igoma umbali wa kilometa nane kutoka katikati ya Jiji la Mwanza.

Hadi sasa hakuna sababu rasmi zilizokwishatolewa na Serikali kuhusu chanzo cha ajali ya MV Bukoba ingawa wapo baadhi ya watu na viongozi wanaosema ilitokana na meli hiyo kujaza abiria na mizigo kupita kiasi, na kwamba ilikumbwa na dhoruba kali ziwani.

Meli hiyo ambayo ilijengwa na kampuni ya Kibelgiji, tangu kuzinduliwa kwake ilikuwa na tatizo la uwiano.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us