Kanda ya Afrika imerekodi kupungua kwa kasi zaidi duniani kwa vifo vya kifua kikuu (TB) tangu 2015, licha ya kuwepo na hatua finyu za kudhibiti maambukizi na vifo, kulingana na Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) Global TB Report 2024.
Ripoti hiyo pia imesema vifo kutokana na TB vilipungua kwa 42% kati ya 2015 na 2023 wakati maambukizi yalipungua kwa 24% katika kipindi hicho.
WHO inasema pia kuwa, huduma ya matibabu ilipanda kutoka 55% hadi 74% kote kanda.
Mwaka huu, Siku ya Kifua Kikuu Duniani inaadhimishwa chini ya kaulimbiu "Ndiyo! Tunaweza Kukomesha Kifua Kikuu: Jitolea, Wekeza, Toa", ambayo inataka hatua za haraka zichukuliwe ili kutimiza ahadi za ufadhili wa vita dhidi ya TB.
Tishio la kurudi nyuma
Hata hivyo shirika la Mkurugenzi wa WHO, Dr Tedros Adhanom Ghebreyesus ameonya kukwama au hata kurudi nyuma kwa hatua zilizopigwa kudhibiti ugonjwa huo katika miaka 20 iliyopita.
Hii ni kutokana na tisho la kupungua maradufu ufadhili, kufuatia hatua ya Donald Trump wa Marekani kukata ufadhili wa Mashirika ya misaada nje ya Marekani, na mpango wa Trump kujiondoa kutoka WHO.
"Mafanikio makubwa ambayo dunia imepata dhidi ya TB katika kipindi cha miaka 20 sasa yako hatarini huku kupunguzwa kwa fedha kunaanza kutatiza upatikanaji wa huduma za kinga, uchunguzi na matibabu kwa watu wenye TB," alisema Dr Tedros.
Dr Tedros alisisitiza haja ya uwekezaji madhubuti na hatua madhubuti za kuongeza afua zinazopendekezwa na WHO za uchunguzi wa mapema, utambuzi, matibabu na kinga wa TB wa hali ya juu.
Nchi zilizopiga hatua kubwa
Afrika Kusini inaongoza kwa kupunguza visa vya Kifua Kikuu kwa zaidi ya 50% kati ya 2015 na 2023, na kuwa nchi ya kwanza katika kanda kupita hatua muhimu ya 2025 mbele ya ratiba.
Msumbiji, Tanzania, Togo na Zambia pia tayari zimefikia lengo la 2025 la kupunguza vifo vya TB kwa 75%.
Nchi nyingine, ikiwa ni pamoja na Kenya, Malawi, Rwanda, Sierra Leone na Uganda zinafuata kwa karibu sana, na kupunguza vifo vya 66% au zaidi.
Katika ngazi ya kanda, Afrika Mashariki na Kusini zimekuwa kichocheo kikuu cha kupunguza TB, na kupunguza matukio kutoka 466 hadi 266 kwa watu 100 000 kati ya mwaka wa 2000 na 2023.
Takwimu za TB Duniani
‘‘Hatuwezi kukata tamaa juu ya ahadi madhubuti ambazo viongozi wa dunia walitoa kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa miezi 18 tu iliyopita ili kuharakisha kazi ya kukomesha TB,’’ ameongeza Dr Tedros.
Japo Afrika imerekodi upungufu wa vifo na maambukizi, bado juhudi zaidi kutokomeza kabisa ugonjwa huo barani huku nje ya Afrika bado maambukizi yanarekodiwa na vifo.
Jumla ya watu milioni 1.25 walikufa kutokana na kifua kikuu (TB) mwaka 2023 kote duniani huku takriban milioni 10.8 waliugua TB katika kipindi hivho. Miongoni mwao ni Wanaume milioni 6.0, wanawake milioni 3.6 na watoto milioni 1.3.
TB inaambukiza kwa haraka sana kupitia hewa japo inaweza kukingwa na kutibiwa hasa ukichunguzwa mapema na kuanza kupokea dawa.