Mnamo Januari 20, 2025, Watanzania waliamka na taarifa za uwepo wa virusi vya ugonjwa wa Marburg katika wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera.
Pamoja na kutangaza uwepo wa virusi hivyo hatari, Wizara ya Afya nchini Tanzania ilifanya jitihada za haraka kudhibiti mlipuko huo, ikishirikiana na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Barani Afrika (Africa CDC) pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Kwa bahati nzuri, mlipuko huo ulidhibitiwa licha ya wagonjwa kadhaa kupoteza maisha.
Taaluma ya kujifundisha
Katika nchi nyingi za Afrika, waganga wa kienyeji wanabaki kuwa kimbilio la kwanza kwa wagonjwa hasa wa maeneo ya vijijini, ambako hospitali ziko mbali.
Taaluma hii huwa ni ya kimapokeo kutoka kwa wazee, ambao hutumia mitishamba.
Lakini ni nini hutokea mgonjwa anapoonesha dalili kali kama vile kutokwa na damu nyingi na homa na maumivu ya mwili? Hivi karibuni Africa CDC ilikutana na Meriam Mapinduzi Kagazi, mganga wa kienyeji wilayani Biharamulo.
"Wengi wetu tulifikiri dalili kama vile kutapika damu au kuharisha ni ishara za uchawi. Sasa, tunajua ni Marburg. Ni kweli, ni hatari na inaweza kuzuiwa,” Kagazi anaeleza.
Daraja kati ya tiba za jadi na za kisasa
Meriam Kagazi ni sehemu ya kikundi cha Waganga wa Jadi waliochaguliwa kupewa mafunzo maalum yaliyoandaliwa na wizara ya Afya nchini Tanzania, Afrika CDC na WHO ili kuimarisha utambuzi wa kukabiliana na magonjwa.
"Kama tungekuwa na vipima joto, tungeweza kuwachunguza watu kabla hata hawajaingiliana na wengine. Vyombo vya ulinzi ni muhimu, sio kwetu tu, bali kwa watoto na familia tunazozihudumia," aliongeza.
Mpango huu unaashiria hatua muhimu katika kuwaunganisha waganga wa tiba asili katika mfumo wa ufuatiliaji wa afya ya umma nchini Tanzania.
Mafunzo hayo yalilenga ufuatiliaji wa kijamii, unaowapa uwezo waganga wa kienyeji kutambua mienendo na dalili zisizo za kawaida za kiafya zinazoweza kuashiria kuibuka kwa magonjwa ya milipuko.
Kuzuia majanga ya afya kitaifa
Kwa kuwapa ujuzi juu ya dalili za ugonjwa, kuzuia maambukizi, na hatua za kudhibiti, mamlaka zinatumai kuunda mfumo wa tahadhari wa mapema ambao unaweza kuzuia milipuko ambayo yanaweza kugeuka kuwa majanga ya kitaifa.
"Waganga wa kienyeji sio walezi tu. Ni walinzi wa afya ya jamii," anasema Peter Mabwe, Mratibu kutoka Wizara ya Afya ya Tanzania. Jukumu lao katika utambuzi wa mapema wa magonjwa na rufaa ni muhimu sana. Kwa kuimarisha ushirikiano huu, tunajenga mfumo ambapo jamii zinaarifiwa, kuitikia, na kushiriki kikamilifu katika kuzuia magonjwa—sio wakati wa milipuko tu,” aliiambia Africa CDC.
Kulingana na Africa CDC, hatua ya kuunganisha waganga wa jadi katika mifumo ya afya ya umma ni uthibitisho wa mkakati muhimu wa kuzuia magonjwa.
Usajili wa waganga wa kienyeji
Na kutokana na kukosa ufadhili kutoka kwa wafadhili wa nje, nchi nyingi kama Tanzania zitajikuta zikienda kwa waganga hawa wa jadi kwa ajili ya kupata msaada katika ngazi ya mashinani.
Jumla ya waganga wa jadi 75, 000 wamesajiliwa nchini Tanzania ili kusaidia kudhibiti tiba hiyo isiyo rasmi.