Taarifa iliyotolewa na ofisi ya msemaji wa serikali siku ya Jumapili, ilisema Rwanda inaunga mkono mipango mingine inayofungua njia kuelekea suluhu la kudumu la kisiasa na kiusalama wa mgogoro unaoendelea katika eneo hilo.
"Rwanda inakaribisha tangazo la M23 la kuondoa vikosi vyake kutoka Walikale ili kuunga mkono mipango ya amani inayoendelea, pamoja na tangazo la DRC kwamba operesheni zote za mashambulizi za FARDC (vikosi vya serikali) na Wazalendo (wanamgambo wanaoiunga mkono serikali) zitasitishwa," ilisema taarifa hiyo.
"Rwanda iko tayari kufanya kazi na pande zote ili kuhakikisha ahadi zilizotolewa zinazingatiwa, hasa katika muktadha wa mchakato wa pamoja wa Mkutano wa wakuu wa EAC-SADC na mipango mingine ambayo itafungua njia kuelekea suluhu la kudumu la kisiasa na kiusalama kwa kanda."
Muungano wa waasi wa Alliance Fleuve Congo unaojumuisha waasi wa M23, ulitangaza Jumamosi nia yake ya "kuondoa" vikosi vyake kutoka mji wa Walikale na maeneo yanayozunguka, ikisema inaunga mkono mipango ya amani inayolenga kuweka mazingira ya mazungumzo ya kisiasa kushughulikia sababu kuu za mzozo mashariki mwa Kongo.
Nafasi ya mazungumzo
Kufuatia tangazo la waasi hao, jeshi la Kongo pia limesema limetoa wito kwa vikosi vya kujilinda vya Kongo kupunguza kasi ili kuipa kipaumbele mazungumzo ya amani na kuendelea kwa mchakato wa mazungumzo ya Luanda na Nairobi.
Tangu kuanza kwa mashambulizi mwaka jana, waasi wa M23 wameteka maeneo muhimu katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.
Congo na nchi nyingine zinaishutumu nchi jirani ya Rwanda kwa kuunga mkono kundi la waasi la M23. Rwanda, hata hivyo, inakanusha madai hayo.
Wiki iliyopita, Rais wa Kongo Felix Tshisekedi na Rais wa Rwanda Paul Kagame walitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano wakati wa mazungumzo ya kupatanishwa na amiri wa Qatar huko Doha.
Mkutano huo ni wa kwanza wa hivi punde zaidi tangu M23 kuteka miji mikuu ya majimbo ya Goma na Bukavu mwaka huu.