Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amedai kuwa Rwanda inapanga njama za kuishambulia nchi yake.
Katika mahojiano yake na chombo kimoja cha habari, Ndayishimiye amesema kuwa ana ushahidi wa kiintelijensia wa Rwanda kuandaa mashambulizi dhidi ya Burundi.
Ndayishimiye alikwenda mbali na kuituhumu Rwanda kuhusika na jaribio la mapinduzi la mwaka 2015.
Hata hivyo, siku ya Jumanne, Rwanda, kupitia Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Olivier Nduhungirehe, ilionesha kushtushwa na madai yaliyotolewa na Rais Ndayishimiye.
"Hakika, kauli ya rais wa Burundi ni ya kushtusha, hususani wakati mamlaka ya nchi hizi mbili zipo katika majadiliano," aliandika Nduhungirehe katika ukurasa wake wa X.
Katika madai yake, Ndayishimiye aliituhumu Rwanda kuhusika na jaribio la mapinduzi la mwaka 2015 la nchini Burundi "kama inavyofanya sasa kwa DRC. "
Rwanda inafahamika kuunga mkono kikundi cha waasi cha M23, ambacho kinadhibiti maeneo nyeti katika eneo la Mashariki mwa DRC.
Mwaka jana, Burundi ililazimika kufunga mpaka wake na Rwanda, baada ya kuituhumu kukiunga mkono kikundi cha RED-Tabara, ambacho ni kikundi cha waasi nchini Burundi.
Katika hatua nyingine, Ndayishimiye amemtaka Rais Paul Kagame kuheshimu mkataba wa amani uliosainiwa miaka ya nyuma na kukabidhi waasi walioshiriki jaribio la mapinduzi la mwaka 2015.