Mwezi Disemba mwaka 2023, niliambatana na mama yangu pamoja na dada zangu kwenda kumuona Gogo Kabon, mama anayesifika kwa dawa za kienyeji, anayeishi katika eneo la Kabarak katika eneo la Ufa la Kenya.
“Huyo mama amenisaidia sana hasa kutibu maumivu yangu ya mgongo, yamepungua tangu nianze kunywa maji ya miti aliyonipa,” alisema mama yangu wakati tukielekea kumuona Kabon.
Mama yangu alikuwa anaenda kumuona Gogo Kabon kwa mara ya pili.
“ Huyu mama anazifahamu vizuri dawa za asili, ni tofauti sana na zile dawa zilizotengenezwa kwa kemikali, hizi hutibu kiasili zaidi,” alisisitiza mama yangu.
Kulingana na mama yangu, mchemsho wa maji ya miti aliyokuwa amepewa na mtaalamu huyo wa tiba asilia, ulikuwa umekwisha “ makali”.
Mama yangu aliniambia kuwa, baada ya kukabidhiwa vijiti hivyo vilianza maji yenye rangi nzito lakini baada ya muda, maji hayo yakaanza kubadilika na na kuwa miepesi, kiashiria cha ‘kupoteza nguvu yake’.
Licha ya kutoweza kuambatana nasi kati safari hiyo, dada yangu mwingine aliomba tumletee dawa kutoka kwa Gogo Gabon.
Imani kwa dawa za asili
Tulipofika kwa Gabon, tulikuta umati wa watu; wakiwa wamekuja na magari yao na wengine kwa miguu. Wengi walilazimika kuketi kwenye nyasi, wakisubiri zamu yao ifike ili wapate kuhudumiwa.
“ Ni mara yako ya kwanza kufika hapa?” nilimuuliza kijana mmoja wa makamo.
“ Hapana, ni mwaka wangu wa tatu sasa. Nimekuwa nikija hapa kuchukua dawa, kwa ajili ya mguu wangu wa kushoto ambao umevimba sana. Dawa nilizopewa hospitali hazijanipa nafuu yoyote, ukilinganisha na miti shamba ya Kabon,” alinielezea.
Mara kwa mara, tulianza kusikia vicheko kutoka kwenye nyumba ya Kabon.
Tukiwa bado tunasubiria zamu yetu, alipita kijana mmoja aliyekuwa amebeba gunia, na mda mfupi baadaye akamwaga vijiti kando ya nyumba hiyo.
“Hiyo ndiyo dawa sasa imekuja kutoka msituni,” alisema mama mmoja kwa furaha.
Furaha ya mama huyo ilidhihirisha imani ya watu hao kwa dawa hizo za asili.
Kumuona Gogo Kabon
Umoja wa Afrika unatambua huduma za watu kama Gogo Kabon ikisema kuwa “dawa ya kiasili sio tu chaguo la afya bali pia ni sehemu muhimu ya utambulisho wetu na uthabiti wetu wa Kiafrika.”
Umaarufu wa Gogo Kabon, hauishii kijijni kwake pekee, bali umevuka mipaka.
Kulingana na wakazi wa eneo lake, wazazi wa Gogo Kabon walikuwa wana uelewa mkubwa wa miti shamba.
“ Sio kila mtu anaweza kufanya kazi anachofanya Kabon,” alisema bibi mmoja kando yetu.
“Kipawa alichonacho kinatokana na urithi,” aliongezea.
Muda mfupi baadaye, wanawake wawili wanatoka kwenye nyumba ya ‘mtaalamu’ huyo.
Gogo Kabon akajongea hadi kwenye eneo lililomwagwa vijiti, akaokota vichache, kabla ya kuvichanganyachanganya na kuviweka kwenye mfuko, na kuwapa wanawake wale wawili ambao walimshukuru kwa bashasha kubwa.
Zamu yetu kufika
Wote tuliinuka na kuingia kumuona Gogo Kabon, tukiwa kama kikundi. Hata hivyo, alitukatalia, akitaka kumhudumia mmoja baada ya mwingine.
Kila aliyetoka kwenye chumba maalumu cha Gogo Kabon, alipewa vijiti kadhaa kwenye lundo la vijiti vilivyoletwa na kijana yule mwenye gunia.
Zamu yangu ilipowadia, sikujua cha kusema, kwani nilikuwa nimesindikiza jamaa zangu tu.
Hata bila kuniuliza mengi Gogo Kabon , mama mcheshi mno, alinikaribisha na kuniomba nilale chali.
Aliniongelesha huku akigusagusa tumbo langu, akiniuliza maswali kadhaa, ikiwemo kama nilikuwa nina watoto, mume na kadhalika.
Baadaye akaniuliza nini ilikuwa shida yangu. Kiukweli sikuwa na changamoto ya kiafya kwani nilikuwa nimesindikiza mama na dada zangu .
“ Nitakupa kitu cha kusafisha damu yako tu,” alinieleza.
Pia alinipa vijiti kadhaa kutoka kwenye lundo lililokuwa limebaki nje ya nyumba.
Licha ya huduma aliyonipa, Gogo Kabon alitaka kulipwa dola 3 za Kimarekani (sawa na Shilingi 500 za Kenya).
Tulipomwambia kuwa kuna dada yetu ambaye alishindwa kuja na alitamani kupata dawa hizo, Gogo Kabon alisisitiza haja ya kuonana na dada yetu kabla ya kumpa dawa yoyote.
“ Mimi sina tamaa ya pesa, nia yangu ni watu wapone,” alituambia.
Matumizi ya dawa ya Gogo Kabon
“Takriban asilimia 40 ya bidhaa za dawa leo zinatokana na maarifa asilia na asilia, ikijumuisha dawa muhimu kama aspirini, artemisinin, na matibabu ya saratani ya watoto,” linasema Shirika la Afya Duniani (WHO).

Katika nchi nyingi za Afrika, waganga wa kienyeji wanabaki kuwa kimbilio la kwanza kwa wagonjwa hasa wa maeneo ya vijijini, ambako hospitali ziko mbali.
Vijiti nilivyopewa nilivichemsha kwenye maji mengi mara kwa mara, na kuviweka ndani ya chupa. Kwa muongozo wa mama yangu nilikunywa kikombe kimoja asubuhi na kingine jioni.
Ilikuwa na ladha kali ila baada ya muda mfupi, ningejisikia vizuri, mwilini na akilini.
Niliendelea kuchemsha mchanganyiko huo hadi ulipoanza kubadilika na kuwa mwepesi na nikaumwaga.
Tayari mama yetu amesema anatungoja tena tumpeleke kwa Gogo Kabon , kwani miti aliyochukua mwisho wa mwaka uliopita unaonekana kuisha makali tena.