Rais wa Marekani Donald Trump ametofautiana na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini kuhusiana na madai ya mateso na mauaji ya wakulima wazungu nchini Afrika Kusini.
Katika kikao chao kilichofanyika ndani ya ofisi ya Trump ya ‘Oval Office’, siku ya Jumatano, Trump alidai kuwa anao ushahidi wa matukio yenye kuwalenga wakulima wazungu nchini Afrika Kusini, ikiwemo uwepo wa makaburi ya wakulima hao.
"Hili ni jambo baya sana. Kuna makaburi zaidi ya 1,000 ya wazungu pale," alisema Rais Trump wakati akicheza video fupi ndani ya ofisi yake.
"Mheshimiwa Rais, walikueleza ni wapi hayo yalitokea?" alihoji Rais Ramaphosa kwa utulivu.
"Hapana,” alijibu Trump, huku Ramaphosa akisisitiza kuwa alitaka kufahamu zaidi kuhusu video hiyo.
"Nilimanisha ni Afrika Kusini,” alisema Trump.
Wakati wa kikao hicho, Rais Trump anadaiwa kumwambia Ramaphosa kuwa serikali yake iliruhusu “kuchukuliwa kwa mashamba ya wakulima wazungu, kutoka jamii ya Kiafrikana kuchukuliwa na kisha kuwauwa wakulima hao”.
Hata hivyo, Ramaphosa alikana madai hayo, akisisitiza kuwa Afrika Kusini inaendelea na jitihada za kupambana na uhalifu.
"Wanaouwawa sio wazungu. Wengi wao ni watu weusi,” alisema Ramaphosa.