Anaitwa Albert William Longomba, almaarufu kama Awilo Longomba, mfalme wa Soukous barani Afrika.
Akiwa amezaliwa jijini Kinshasa ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, miaka 63 iliyopita, Awilo Longomba anatokea familia ya kimuziki.
Baba yake mzee Vicky Longomba alikuwa muimbaji kiongozi wa kundi la TP OK Jazz la nchini DRC, wakati kaka yake Lovy Longomba Sr, alikuwa sehemu ya bendi ya Super Mazembe.
Awilo alikuwa mjomba kwa Elly Longomba, Christian na Lovy wa kundi la ‘Longombas’ lililowahi kutamba nchini Kenya miaka ya nyuma.
Pia ni mjomba wa mchezaji wa zamani wa Ufaransa na Chelsea ya Uingereza, Claude Makelele.
Awilo alijiunga na kundi la Viva La Musica lililokuwa likiongozwa na Papa Wemba, ambapo Awilo alihudumu kama mpiga ngoma wa bendi hiyo.
Mwaka 1991, alianzisha kundi lake mwenyewe lililoitwa Nouvelle Génération, yaani ‘Kizazi Kipya’, akiwa na nyota wengine kama vile Luciana de Mingongo na Lidjo Kwempa.
Kundi hilo lilipata umaarufu kupitia mtindo wake ‘Zipompa-pompa’.
Awilo alipewa uraia wa Ufaransa, baada ya kumuoa mwanamke wa Kifaransa mwaka 1994.
Awilo, ambaye anajulikana kwa mtindo wake kupiga kelele wakati anaimba, aliachana na ‘Nouvelle Génération’ mwaka 1995, na kuamua kujitegemea, kabla hajafyatua albamu yake ya kwanza ya ‘Moto Pamba’.
Mwaka 1996, Awilo alitwaa tuzo ya Msanii Bora wa Afrika ya Kati, na mwaka 1997, akashinda KORA Awards.
Mwaka 2019 alipata Legend Award ya AFRIMA, huku mwaka 2025 akiwa ameorodheshwa kama mtumbuizaji bora Afrika.
Mwaka 1998, akatoa ‘Coupe Bibamba’ ambayo ilibamba vilivyo enzi hizo, ikisheheni nyimbo kama vile ‘Gâté le coin’, ‘Mobimba ya Mama’ na ‘Coupé Bibamba’ yenyewe.
Awilo alifanya ziara za kutosha ukanda wa Afrika Mashariki na hata Ulaya.
Albamu yake ya tatu iliitwa ‘Kafou Kafou’ kabla ya kuachia ‘Mondongo’ mwaka 2004, iliyokuwa na wimbo maarufu wa ‘Karolina’, albamu ambayo ilikuja kuuza zaidi ya nakala elfu 30 nchini Ufaransa.
Novemba 2022, Awilo alishirikiana na wanamuziki wengine kama vile M'bilia Bel, Werrason, Reddy Amisi na Jossart N'Yoka Longo kutoa wimbo maalumu wa kuhimiza wacongo kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2023.
Kwa sasa, mfalme huyo wa techno soukous amehamishia makazi yake Ulaya.