Katika jamii ya Giriama inayopatikana katika eneo la pwani ya Kenya, jina la Mekatilili wa Menza limejizoelea umaarufu.
Hakuwa mtu wa kawaida. Alikuwa ni ishara ya nguvu na ushupavu, aliyepambana na ukandamizwaji uliofanywa na wakoloni wa Uingereza.
Kenya ilikabiliwa na utawala wa kikoloni kutoka kwa Waingereza kuanzia mwaka 1895 hadi 1963, huku jamii mbalimbali zikijaribu kupambana na utawala huo.
Kati ya jamii hizo ni pamoja na Wagiriama, ambao ni sehemu ya Wamijikenda, wakiongozwa na Mekatilili wa Menza.
Kuwasili kwa ‘wazungu’
Akiwa amezaliwa mwaka 1840 huko Kilifi, Mekatilili alijulikana kama Mnyazi wa Menza, mara tu baada ya kuzaliwa.
Hata hivyo, alibadili jina lake na kuitwa Mekatilili, likimaanisha “mama wa Katilili”, baada ya kupata mtoto wa kwanza.
Akiwa angali binti mdogo, Mekatilili alisikiliza simulizi kutoka kwa bibi yake kwa shauku kubwa sana, akitaka kufahamu mtindo wa maisha wa jamii ya Wagiriama.
Kilichomvutia zaidi ni simulizi ya nabii wa kike wa Kigiriama aitwaye Mepoho, ambaye aliweza kutabiri ujio wa “wazungu” katika pwani ya Kenya.
Kulingana na utabiri huo, ujio wa wageni ungesababisha watu wa Giriama kupoteza ardhi na uhuru wao.
Katika utabiri wake, Mepoho alisema kuwa ataibuka mwanamke shupavu katika jamii ya Wagiriama ambaye atapambana dhidi ya ukandamizwaji huo, bila Mekatilili mwenyewe kubaini kuwa ni yeye aliyekuwa akizungumziwa.
Kiongozi na mpiganaji
Katika ujana wake, Mekatilili alijishughulisha zaidi na biashara, akisafiri kwenda Malindi. Kituo chake kikuu cha biashara kilikuwa ni soko la Takaungu karibu na Kilifi, ambapo alikutana na walowezi wa Kiingereza.
Ilipofika mwaka 1895, Kenya ikawa chini ya utawala wa Waingereza.
Wakoloni hao walifahamika kwa kuteka watu na kwenda kuwatumikisha, wakifanya hivyo kwa kaka wa Mekatilili, aitwaye Mwarandu.
Tukio hili lilimkera sana Mekatilili na hapo ndipo ujasiri wa kupambana na utawala wa Waingereza ukamuingia.
Mekatilili alianza kukusanya jamii yake ili ipambane na manyanyaso ya Waingereza. Alitumia nyimbo za ngoma na nyimbo za kitamaduni kama nyenzo ya mawasiliano.
Kwa kuwa alikuwa mjane, Mekatilili alikuwa na nafasi ya kipekee sana katika jamii ya wamijikenda.
Kupinga manyanyaso
Mwezi Agosti 1913, Mekatilili, bila hofu yoyote ‘alimvaa’ mtawala wa Kiingereza katika eneo hilo kwa wakati huo, aliyejulikana kama Arthur Champion.
Alivamia kikao kilichokuwa kikiendeshwa na Champion mwenyewe, na kumzaba kibao mzungu huyo na maofisa wengine.
Jambo hilo liliwashtua Waingereza na kuanza kumfuatilia kwa ukaribu.
Hata hivyo, kadiri walivyojaribu kumkandamiza, ndivyo walivyozidi kumuongezea umaarufu.
Mara baada ya kukabiliana na Champion, Mekatilili alikusanya jamii ya Wagiriama katika kikao maalumu kilichofanyika kwenye mji wa Kilifi, ambapo wazee wa jadi waliapa kutokushirikiana na Waingereza.
Kufungwa jela na kutoroka
Kama kisasi, Waingereza walitwaa sehemu kubwa ya ardhi ya Wagiriama, kuhamisha watu na familia zao.
Pia waliweza kuwauwa zaidi ya watu 150 na kuchoma makazi 5,000.
Ilipofika Oktoba 1913, Mekatilili na kiongozi wa jamii aliyejulikana kama Wanje wa Mwadorikola, walikamatwa na kupelekwa katika mji wa Kisii ambapo walifungwa.
Hata hivyo, ilipofika mwezi Aprili 1914, wawili hao walifanikiwa kutoroka kutoka kifungo hicho na kuanza safari ndefu ya kurudi Kilifi.
Akiwa nyumbani, Mekatilili aliendeleza mapambano dhidi ya Waingereza.
Ushindi na kujiondoa kwa Waingereza
Oktoba 1914, jamii ya Wagiriama walianzisha shambulizi kubwa lililosababisha vifo vingi.
Hata hivyo, vita vya kwanza vya dunia (1914-1918) vilidhoofisha rasilimali za Waingereza katika mapambano hayo, hali iliyomfanya Arthur Champion asalimu amri.
Jamii ya Giriama iliruhusiwa kuanzisha mifumo yao ya uongozi huku Mekatilili akichaguliwa baraza la wanawake huku Wanje akiongoza baraza zima la Wagiriama.
Mekatilili alifariki dunia katikati ya miaka ya 1920, huku jina lake likiwekwa kwenye orodha ya mashujaa waliowahi kuishi nchini Kenya.