Naibu Rais wa Sudan Kusini ambaye pia ni kiongozi wa chama cha upinzani SPLM/IO Riek Machar, ametaka majeshi wa Uganda kuondoka nchini humo.
“Katika barua aliyoituma kwa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Kikanda ya IGAD, Machar alisema uingiliaji wa kijeshi wa Uganda nchini Sudan Kusini umekiuka makubaliano ya amani ya mwaka 2018, ambayo yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano.
Uganda ilisema kuwa ilituma wanajeshi wake nchini Sudan Kusini mapema mwezi huu kufuatia ombi la serikali baada ya kuvunjika kwa uhusiano kati ya Machar na Rais Salva Kiir.
“Jeshi la Uganda liliingia Sudan Kusini likiwa na vikosi kamili vya jeshi la anga na kukiuka azimio nambari 2428 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la Julai 13, 2018 lililoongezwa Mei 30, 2024 kwa mwaka mmoja,” Machar alisema katika taarifa yake.
Machar amesema kuwa mkataba kati ya serikali ya Sudan Kusini na Uganda ulifanyika kabla ya serikali ya mpito kuundwa 2018 kwa hivyo haina uzito.
“Mkataba kati ya serikali ya Sudan Kusini na Uganda inayojulikana kama makubaliano ya hali ya vikosi kati ya serikali ya Uganda na serikali ya wakati huo ya Sudan yalitiwa saini tarehe 10 Januari 2014,” Machar ameelezea.
“Makubaliano hayakutiwa saini na serikali ya mpito iliyohusishwa ya Umoja wa Kitaifa na kwa hivyo makubaliano (mapya ya serikali ya mpito ya 2018) yanachukua nafasi ya kwanza kuliko makubaliano hayo ya kijeshi,” ameongeza.
Machar anadai kuwa mzozo katika eno la Nasir Unaweza kutatuliwa kwa utulivu kupitia mchakato wa usalama wa mpito hasa bodi ya pamoja wa usalama, ambayo ina jukumu la majeshi yote na hivyo haihitaji vikosi kutoka nje.
“Kuna hofu kwa upande wetu kwamba makubaliano yetu ya amani ya 2018 huenda yamefeli kwa sababu ya masuala kama uingiliaji wa Uganda.
“Kwa hivyo tunaomba Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika, Shirika la Kikanda la IGAD na Baraza la Uslaama la Umoja wa Mataifa kuingilia kati na kuiambia Uganda kuondoa majeshi yake.