Hatua hiyo ya FKF inakuja baada ya video moja iliyoibuka mtandaoni ikimuonesha mlinda mlango huyo akijadili kuhusu njama na watu wasiojulikana ya kupanga mechi ya soka.
FKF imethibitisha kufahamu kuhusu video hiyo, na kusisitiza kuwa madai hayo wanayashughulikia kwa ushirikiano wa shirikisho la soka duniani FIFA, na lile la Afrika CAF, pamoja na mashirika mengine husika.
“Tunapenda kuthibitisha msimamo wetu thabiti kuhusu upangaji wa mechi na tuna nia ya kulinda uaminifu wa mashindano yetu.” FKF imesema katika taarifa hiyo.
Taarifa hii imetolewa baada ya wadau wa soka nchini Kenya, kutoa hisia zao kali katika mitandao ya kijamii kufuatia video inayodaiwa kumuonesha kipa Patrick Matasi akizungumzia ‘dili’ la kupanga mechi.
Wengine waliokuwepo kwenye video hiyo hawakuonekana vizuri, isipokuwa sura ya mchezaji huyo imetambuliwa.
Matasi amekuwa mlinda mlango anayetegemewa wa timu ya taifa ya Kenya kwa muda mrefu. Lakini tangu kuja kwa kocha mpya Benni McCarthy, anaonekana kupoteza nafasi hiyo na badala yake Ian Otieno ameaminiwa kuwa kipa namba moja wa Harambee stars.