Kocha wa Inter Milan, Simone Inzaghi, amewapongeza wachezaji wake kwa ushupavu waliouonyesha baada ya kuiondoa Barcelona katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa ushindi wa jumla wa mabao 7–6, katika mchezo wa kusisimua uliodumu hadi dakika za mwisho.
Inzaghi amesema anajivunia sana mafanikio ya timu yake, hasa baada ya kuizidi nguvu miamba wawili wa Ulaya.
Katika robo fainali, Inter waliwatupa nje Bayern Munich ya Ujerumani, kabla ya kuwazidi Barcelona kwenye nusu fainali.
Ingawa Barcelona walikuwa mbele kwa mabao 3–2, Inter walionyesha moyo wa kupambana na kusawazisha dakika za majeruhi kupitia Francesco Acerbi.
Bao la ushindi lilifungwa na Davide Frattesi katika muda wa nyongeza, na kuwapeleka Inter kwenye fainali.
Inter Milan sasa wanasubiri mshindi kati ya Paris Saint-Germain na Arsenal, watakaokutana nao katika fainali itakayochezwa tarehe 31 Mei kwenye uwanja wa Allianz Arena, Ujerumani.