AFRIKA
3 dk kusoma
Siasa za Sudan Kusini: Ni nani Riek Machar?
Hali ya hofu imetanda nchini Sudan Kusini na majirani huku ripoti kutoka nchi hiyo zikiashiria kuzuiliwa na maafisa wa usalama kwa Makamu wa Rais Riek Machar
Siasa za Sudan Kusini: Ni nani Riek Machar?
Makamu wa Rais wa Sudan Kusini Riek Machar amezuiliwa na maafisa wa usalama / Reuters
27 Machi 2025

Kufuatia Sudan Kusini kupata uhuru mwaka 2011, Machar alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri Huru ya Sudan Kusini huku Salva Kiir akiwa Rais.

Lakini historia yake wa siasa ilianza wakati ambapo Sudan Kusini ilikuwa bado haijajitenga na Sudan.

Machar anatoka katika kabila la Nuer, ambalo lilipigana vikali na kabila kubwa la Dinka nchini humo, ambalo Rais wa nchi hiyo Salva Kiir anatoka, mwanzoni mwa miaka ya 1990 wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan.

Kuanzia 1984, Machar alikuwa kiongozi wa waasi wa Sudan People’s Liberation Army/Movement (SPLM/A), ambayo iliongoza vita vya kupigania uhuru wa Sudan Kusini kutoka kaskazini.

Vuguvugu hilo iliongozwa na marehemu John Garang, ambaye alitambulika na watu wa Sudan kaskazini na kusini kwa maono yake ya "Sudan mpya."

Garanga alitaka Sudan ambayo ilikuwa na umoja, isiyo ya kidini na yenye haki sawa kwa wote.

Kinyume chake, Machar mara zote alikuwa akitoa wito wa kujitawala kwa upande wa kusini.

Baada ya kutofautiana na Garang mwaka wa 1991, alijitenga na SPLM/A na kuunda kundi lake la kujitenga, lililoitwa SPLA-Nasir.

Mapigano makali kati ya vikosi vya Machar na SPLA yaliibuka.

Machar na makundi yake yalipata msaada kutoka kwa serikali ya Sudan na mwaka 1997, alitia saini mkataba na Khartoum na kuwa msaidizi wa Rais wa wakati huo wa Sudan Omar al-Bashir.

Hata hivyo, miaka michache baadaye, alirudi kwa waasi, akarekebisha uhusiano na Garang na kujiunga tena na SPLA kama kamanda mkuu mnamo 2002.

Baada ya makubaliano ya amani ya 2005 ambayo yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuanzisha mikakati ya uhuru wa kusini, Machar alikua makamu wa rais wa Kusini, akidumisha jukumu hili baada ya uhuru rasmi mnamo 2011, hadi kufukuzwa kwake.

Kama kiongozi wa SPLA-Nasir, Machar alihusishwa na mauaji ya Bor 1991, ambapo watu 2,000, wengi wao wakiwa raia wa Dinka waliuawa.

Mnamo 2012, aliomba msamaha hadharani kwa kuhusika katika maafa hayo.

Siasa baada ya vita

Kufuatia Sudan Kusini kupata uhuru mwaka 2011, Machar alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri huru ya Sudan Kusini huku Salva Kiir akiwa Rais.

Vita vilivyotokea kwa sababu ya mvutano wa kisiasa baina yake na Rais Kiir viliingiza nchi hiyo changa kabisa Afrika katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Makubaliano ya amani kati ya serikali ya Rais Kiir, mrengo wa Machar na wadau wengine ulifanyika 2018.

Makubaliano hayo yalikuwa ndio msingi wa kuundwa kwa seriklai ya mpito nchini humo.

Mnamo Februari 2020, Machar aliapishwa tena kama makamu wa kwanza wa rais kufuatia makubaliano hayo.

Yeye pia ni mkuu wa kundi linalojulikana kama SPLM-IO (Sudan People's Liberation Movement-In Opposition) mrengo wa upinzani kutoka chama tawala, ambao aliuanzisha mwaka 2014 kufuatia kuzuka kwa vita vya 2013.

Maisha yake ya familia

Machar alizaliwa Leer, Jimbo la Unity mwaka 1953.

Alisomea uhandisi katika Chuo Kikuu cha Khartoum na alitunukiwa PhD katika falsafa na Mipango ya Kimkakati kutoka Chuo Kikuu cha Uingereza cha Bradford mnamo 1984.

Mnamo 1991 alimuoa Emma McCune, mfanyakazi wa misaada wa Uingereza wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe ambaye alifariki katika ajali ya gari akiwa mjamzito huko Nairobi mwaka wa 1993.

Kwa sasa Machar amemuoa Angelina Teny, mwanasiasa maarufu Sudan Kusini.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us