Ziwa Assal Djibouti, sehemu ya chini zaidi ya usawa wa bahari Afrika
Ziwa Assal Djibouti, sehemu ya chini zaidi ya usawa wa bahari Afrika
Hii ndio sehemu ambayo iko chini zaidi ya usawa wa bahari Afrika ikiwa takriban mita 153 na ni eneo la tatu duniani, baada ya Bahari ya Chumvi na Bahari ya Galilaya.
24 Machi 2025

Ijapokuwa maziwa mingi yamejaa mimea na viumbe hai, hali ni tofauti kwa Ziwa Assal lililopo nchini Djibouti ambalo lina chumvi nyingi isiyoruhusu viumbe kuishi. Hili ni mojawapo ya maziwa yenye chumvi nyingi zaidi duniani.

Ziwa Assal ni volkeno ya kipekee, lenye umbo la mviringo. Liko katikati-magharibi mwa Djibouti, mwisho wa magharibi wa Ghuba ya Tadjoura katika Mkoa wa Tadjoura. Eneo la maji ya Ziwa ni kilomita za mraba 900.

Ziwa hilo lina urefu wa kilomita 19 na upana wa kilomita 6.5, lina kina cha takriban mita 40 huku likizungungukwa na volkeno zisizo hai. Kuna sehemu mbili tofauti za ziwa, sehemu kavu na ile yenye maji yaliyojaa chumvi.

Sehemu kavu ya Ziwa ni matokeo ya kukauka kwa maji kutokana na mvuke wa jua. Hii imeacha eneo la chumvi lililo wazi upande wa magharibi-kaskazini-magharibi mwa ziwa.

Likiwa katika jangwa, majira ya joto katika ziwa hufikia mpaka nyuzi joto 52 kuanzia mwezi Mei hadi Septemba.

Majira ya baridi kali ni kuanzia mwezi Oktoba hadi April ambapo kiwango cha joto hufikia nyuzi joto 34. Ziwa Assal halina sehemu ya maji yanayotiririka.

Maji yote ya ziwa hujikusanya ndani ya volkeno ya Ziwa.

Maji ya bahari kutoka kwenye chemchemu za jotoardhi ndiyo huingia kwenye Ziwa Assal.

Ziwa Assal ni chanzo kikubwa cha uvunaji wa chumvi nchini Djibouti. Lakini pia maji hayo yana madini mengine mengi ambayo yanafaa kwa ngozi kama vile magnesiamu, kalsiamu na salfati, hivyo kulifanya Ziwa Assal kuwa sehemu ya utajiri muhimu wa Afrika.

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us