Kiongozi wa upinzani nchini Msumbiji Venancio Mondlane na Rais wa nchi hiyo Daniel Chapo, siku ya Jumatatu walikubaliana kumaliza machafuko nchini humo, ambaye yamehusisha waandamanaji na vikosi vya usalama kwa miezi kadhaa sasa.
Wawili hao walikutana siku ya Jumapili katika mji mkuu wa nchi hiyo Maputo.
Nchi hiyo imekumbwa na machafuko ya kisiasa tangu kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa mwezi Oktoba mwaka 2024.
"Tutamaliza machafuko hayo," alisema Mondlane katika picha mjongeo iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
"Ni muhimu kwa pande zote kumaliza utesaji huu."
Kulingana na Mondlane, vitendo hivyo vinahusisha utesaji kutoka kwa polisi dhidi ya raia, na vurugu dhidi ya poliis pamoja na wafuasi wake na wale wa chama tawala, alisema Mondlane.
"Ni lazima tudhibiti uharibu wa mali za umma na za watu binafsi ... ili kuipa nchi yetu nafasi ya kutulia," alisema.
Zaidi ya watu 360 wamepoteza maisha kupitia maandamano, kulingana na asasi ya kiraia nchini humo.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa upinzani, kiongozi wa nchi hiyo pia ameridhia kutoa msaada wa “kisaikolojia” kwa familia za waathirika wa vurugu hizo.