Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki-EAC na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika-SADC wamewateuwa marais wastaafu wengine kuongoza jitihada za amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Mkutano huo uliongozwa na Rais Willam Ruto wa Kenya na Emmerson Mnangagwa katika nyadhifa zao kama Mwenyekiti wa EAC na SADC, mtawalia.
Mashambulizi ya kikundi cha M23 mashariki mwa DRC yamesababisha mauaji ya maelfu huku wengine kuyahama makazi yao .
Mapigano hayo pia yamezua upya mvutano kati ya DRC na Rwanda, huku Rwanda ikilaumiwa kwa kuiunga mkono M23, tuhuma ambazo imekana.
Wawezeshaji wapya ni Kgalema Motlanthe wa Afrika Kusini, Catherine Samba Panza kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sahle-Work Zwelde Rais wa zamani wa Ethiopia.
Jopo hilo litafanya kazi pamoja na Uhuru Kenyatta wa Kenya na Olusegun Obasanjo wa Nigeria ambao awali walikuwa wametajwa kuwa wawezeshaji wa juhudi za amani.
Safu mpya, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa baada ya mkutano, ilikubaliwa na mkutano wa marais baada ya kuzingatia jinsia, eneo na ushirikishwaji wa lugha.
Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia Hailemariam Desalegn ambaye hapo awali alikuwa ametajwa kuwa miongoni mwa wawezeshaji hakujumuishwa kwenye orodha mpya ya wawezeshaji.
Wakati huo huo, mkutano huo, ambao ulihudhuriwa na Rais Paul Kagame wa Rwanda na Felix Tshisekedi wa DRC ulipitisha mpangilio ulioandaliwa wiki iliyopita na wakuu wa jeshi kutoka kambi hizo mbili ambao ulielezea kwa kina hatua za haraka, za kati na za muda mrefu ili kufikia amani na usalama endelevu nchini DRC.
Wakuu hao wa jeshi walikutana wiki iliyopita katika mji mkuu wa Zimbabwe Harare na mkutano wao ulifuatiwa na wa mawaziri husika wa Mambo ya Nje na Ulinzi.
Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika zilipewa mamlaka na Umoja wa Afrika kuongoza katika mchakato wa kupunguza hali ya wasiwasi nchini DRC baada ya waasi wa M23 kuvivamia vikosi vya serikali ya DRC na muungano wa makundi ya wanamgambo, ikiwemo mauaji ya halaiki FDLR na kuteka maeneo tofauti mashariki mwa nchi hiyo.