Wizara ya Utalii Kenya inasema mashindano ya kimataifa ya magari yaani World Rally Championship yaliyofanyika mjini Naivasha kuanzia Machi 20 hadi 23, 2025, yamevutia wageni zaidi tofauti na mashindano ya miaka mitatu iliyoopita.
“Imevumbua upya utalii wa michezo nchini mwetu. Mwaka huu watu wamekuwa wengi. Kwa siku tatu watu 400,000 wameweza kuja moja kwa moja kujiunga na msisimko wa rally,” amesema Waziri wa Utalii wa Kenya Rebecca Miano.
Serikali imesema zaidi ya mashabiki kutoka nchi 40 walihudhuria huku nchi jirani za Afrika Mashariki zikichangia wageni takriban 30,000,” Miano amesema.
Kandarasi mpya
Shirika la WRC limesema litaendeleza ushirikiano wake na Safari Rally Kenya na mazungumzo kuhusu kandarasi mpya ya muda mrefu na serikali ya Kenya yanaendelea.
Simon Larkin, Promota Mkuu wa WRC, alitangaza kuwa pia wamezungumza na makampuni kadhaa mashuhuri nchini Kenya ili kupanua ushiriki wao katika hafla hiyo.
"Kwa hakika hakuna shaka kuhusu hilo lakini tuna historia na Safari Rally Kenya ya kuhakikisha kwamba tunafanya upya kandarasi mapema. Tunaona tukijitolea kwa muda mrefu hapa Kenya," Larkin alisema.
Mkataba wa sasa kati ya Safari Rally na WRC unamalizika 2026 baada ya Promota na serikali kukubaliana kuongeza mwaka mmoja kwa kandarasi ya awali ya miaka mitano iliyoanza 2021.
Kenya imesema inafuatilia kuingia mkataba wa kuhakikisha mashindano ya kila mwaka ya Safari Rally kama sehemu ya Kalenda ya Ubingwa wa Dunia (WRC) zaidi ya mwaka ujao.
"Hili ni jambo ambalo tumekuwa tukishughulikia na Rais William Ruto na Katibu wa Baraza la Mawaziri kwa muda sasa. Tumekuwa na ahadi ya muda mrefu hadi sasa na tuna kandarasi ya 2026,” Mvurya amesema.
Mkurugenzi wa Matukio ya WRC, Larkin alifichua kuwa mazungumzo na Kenya ili kuongeza kandarasi na Safari Rally yalianza baada ya toleo la mwaka jana, toleo la nne tangu WRC iliporejea nchini Kenya mwaka wa 2021, baada ya kutokuwepo kwa miaka 19.
Sekta binafsi iandae mashindano
Baada ya miongo kadhaa ya kuwa katika kalenda ya kimataifa, Safari Rally Kenya iliondolewa kwenye kalenda ya kimataifa mwaka 2002 kutokana na kushindwa kupata dhamana ya serikali kufadhili tukio hilo.
20 Machi 2024, katika ufunguzi wa mashindano hayo yaliyokamilika 23 Machi 2024, Rais William Ruto alisema kuwa hafla hiyo inafaa kufanywa hasa na sekta binafsi.
Mwaka huu gharama ya kuandaa mashindano hayo imekuwa zaidi ya dola milioni saba, huku Rais amesema inafaa kupungua zaidi kwa sekta binafsi kuingilia kati, ili kuiokoa serikali na fedha inazotumia.
Wizara ya Utalii inasema zaidi ya wageni 40,000 kutoka Afrika Mashariki na kwengineko, walihudhuria huku shindano hilo likihusisha mataifa 20 na washiriki 48 wa mashindano.
WRC inasema tayari imeanza kufanya maongezi na washirika wa kampuni waliopo kwenye Safari Rally ikiwa ni pamoja na watoa huduma jumuishi wa mawasiliano, Safaricom, Benki ya Biashara ya Kenya (KCB) na Shirika la Ndege la Kenya Airways miongoni mwa wengine.
"Huu ndiyo mustakabali wa hafla hiyo na ni jinsi tunavyoweza kuitangaza kibiashara zaidi. Tunafikiri kuna fursa kubwa zaidi ya utangazaji nchini Kenya,” Larkin amesema.