Wabunge kadhaa nchini Uganda wamependekeza kuweka kipaumbele katika marekebisho ya Sheria ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF), 2005.
Waziri Kivuli wa Ulinzi Derrick Nyekho amesema hii itatoa muelekezo mpya wa kuhakikiwa kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) na Naibu wake na Bunge, ili kujua uwezo na uadilifu wao kabla ya kushika madaraka, kama ajenda kuu ya Upinzani mwaka 2025/26.
"Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Naibu, hawachunguzwi na chombo chochote ili kuhakikisha ustadi, uwezo na uadilifu wa mtu aliyeteuliwa kuhudumu katika nafasi hiyo. Si ajabu nidhamu ya jeshi la UPDF inaendelea kutiliwa shaka,” Nyekho aliliambia Bunge.
Pendekezo lake liko katika Taarifa ya Sera Mbadala ya Mawaziri wa Sekta ya Ulinzi ya mwaka 2025/26, ambapo alihoji kwa nini Inspekta Jenerali wa Polisi na Kamishna wa Magereza wanachunguzwa na Bunge, lakini Mkuu wa Jeshi hahusiki na aina yoyote ya uchunguzi huru na chombo chochote cha umma.
“Kuwa na mtu yeyote ambaye hajahakikiwa na chombo huru ili kubaini uwezo wake, uadilifu na ustadi wa kukaimu nafasi hiyo ni kinyume na kanuni ya Katiba na Sheria ya UPDF ya 2005 ya kutoa idhini ya bunge ya wateule wa nyadhifa za Mkuu wa Jeshi na Naibu wake,” Nyekho.
Kwa sasa, chini ya Kifungu cha 8(2)(a) cha Sheria ya jeshi la Uganda, UPDF, Mkuu wa Jeshi anateuliwa na Rais pekee bila aina yoyote ya uhakiki huru.
Machi 2024 Rais wa Uganda Yoweri Museveni alimteua mwanawe, Muhoozi Kainerugaba, kuwa Mkuu wa Jeshi.
Pili katika ajenda ya upinzani wa mwaka ujao ni kuongeza uwajibikaji na uwazi katika jeshi, hasa kwa matumizi yasiyotajwa.
"Wakati uwekezaji katika usalama wa taifa ni muhimu, kuna uwazi mdogo katika jinsi fedha hizi zinavyotumika. Kesi za ukiukwaji wa taratibu za manunuzi, kandarasi zilizopanda, na ukosefu wa uwajibikaji katika matumizi ya kijeshi huibua wasiwasi kuhusu usimamizi wa fedha,” ameambia bunge.