Makubaliano ya DRC-Rwanda: Kwa maslahi ya amani au Maslahi ya Marekani kupata madini?
AFRIKA
5 dk kusoma
Makubaliano ya DRC-Rwanda: Kwa maslahi ya amani au Maslahi ya Marekani kupata madini?Serikali ya Trump imefanya diplomasia ya madini kama sehemu ya sera yake kuu ya mambo ya nje.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC Therese Kayikwamba Wagner (Kushoto) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Olivier Nduhungirehe wakati wa kutia saini makubaliano ya awali 25 Aprili, 2025 Washington, DC. /Getty
6 Mei 2025

Mshauri mwandamizi wa Marekani kuhusu masuala ya Afrika alisema siku ya Jumatatu kuwa amepokea muswada wa awali kutoka kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda kuhusu makubaliano ya amani yatakayomaliza mapigano mashariki mwa DRC.

Akipongeza kuhusu hatua hiyo ya makubaliano ya amani, Massad Boulos alisema kwenye mtandao wa X: ‘’Hii ni hatua muhimu katika kutekeleza ahadi iliyotolewa kwenye azimio.’’

Hata hivyo, iliotajwa kuwa upatanishi uliofanywa na Marekani, unakabiliwa na changamoto, huku wakosoaji wakieleza kuhusu nia ya Marekani ya kutumia vita kwa lengo la kufaidi madini muhimu ya nchi hiyo.

Mshauri mwandamizi wa masuala ya Afrika wa rais Donald Trump Massad Boulos alieleza wiki iliopita kuwa kupata fursa ya kuingia katika sekta ya madini nchini DRC, ambayo kwa sasa inadhibitiwa na China, ni sharti muhimu kwa makubaliano ya amani.

‘Njama fiche’

‘’Tunapotia saini makubaliano ya amani ... makubaliano ya madini na DRC yatatiwa saini pia siku hiyo, na mkataba kama huo, lakini wa aina tofauti, utatiwa saini siku hiyo na Rwanda," Boulos alisema katika mahojiano na shirika la habari la Reuters.

Massad Boulos anasema makubaliano hayo yanaweza kukamilika katika kipindi cha miezi miwili ijayo, huku kukiwa na taarifa kuwa Ikulu ya Marekani inaandaa hafla ya kutia saini mikataba hiyo.

‘’Bila shaka, hili litafanikiwa, alafu unaweza kusema Marekani inataka kumaliza vita na kuona kuwa kanda hiyo inaimarika kiuchumi,’’ Mwanasayansi wa siasa raia wa Rwanda Ismael Buchanan ameiambia TRT Afrika.

‘’Lakini kwa upande mwingine, inaweza kuwa na agenda fiche ya kuwaondoa Wachina, Warusi na wengine. Hilo halina shaka kuwa wanataka kudhibiti sekta nzima ya madini hasa unapozungumzia madini ambayo yako DRC,’’ aliongeza.

Diplomasia ya madini

Serikali ya Trump imefanya diplomasia ya madini kama sehemu muhimu ya sera yake ya mambo ya nje. Imeshasaini makubaliano na Ukraine kuhusu madini yake na pia kuonesha nia ya kufaidi raslimali za Greenland.

Mashariki mwa Congo imebarikiwa na madini adimu yenye thamani ya mabilioni ya madola, ikiwemo kobalti na lithium, ambayo ni muhimu kwa teknolojia ya nishati safi. China inadhibiti sekta ya madini nchini DRC.

Lakini kanda hiyo pia inakabiliwa na mapigano ya miongo kadhaa ambayo yananasibishwa na historia ya nchi hiyo baada ya ukoloni ambapo mataifa ya magharibi yanaingilia masuala ya ndani ya taifa hilo na athari za mauaji ya halaiki ya Rwanda ya 1994. 

Nini kimejadiliwa kufikia sasa?

Kabla ya Marekani kuingilia, mwezi Machi Qatar ilikuwa imewakutanisha katika kikao kilichowashangaza wengi Rais wa DRC Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame. Viongozi hao wawili walieleza nia yao ya kusitisha mapigano na majadiliano ya kumaliza vita kabisa, kulingana na taarifa ya pamoja.

Mikutano mingine ikafuata Doha kati ya maafisa wa Congo na wawakilishi wa muungano wa wapiganaji kwa lengo la kumaliza mapigano kwa amani. Alafu mwishoni mwa mwezi Aprili, mawaziri wa mambo ya nje wa Congo na Rwanda wakakutana jijini Washington kutia saini muongozo wa kuelekea kupata amani.

Kila nchi iliahidi kuheshimu mipaka ya jirani yake na uhuru wa taifa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alisaini kama shahidi lakini mawaziri hao wawili hawakupeana mikono kama ilivyo kawaida wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari.

“Nchi zote mbili (DRC na Rwanda) zimekubaliana kuacha kuunga mkono makundi yenye silaha ambayo yametatiza kanda hiyo na kutoa kipaumbele kwa kurejeshwa kwa wakimbizi wa Congo walioondoka katika makazi yao kutokana na vita,’’ alisema Buchanan.

 Watu wanasema nini kuhusu mazungumzo haya?

Watu wengi wanaonesha kutoridhika na jukumu la Marekani kama mpatanishi mashariki mwa Congo na kote barani Afrika, ambayo wengi wanaona ni mpango wa watu wachache wenye uwezo na utakaosababisha kuanza kupora tena mali ya bara hilo.

“Mazungumzo haya hayamsaidii mtu yoyote. Rais Tshisekedi ameanzisha mazungumzo nyumbani kutafuta suluhu ya nyumbani, kwa sababu suluhu ya matatizo ya ukosefu wa usalama Congo tunaifahamu,’’ Clovis Mutsuva, mwanaharakati wa haki za binadamu mashariki mwa Congo, ameiambia TRT Afrika.

Inaonesha namna gani watu hawaamini mataifa ya kigeni kuingilia kati, ambayo kama tulivyoona hivi karibuni mamluki kutoka Romania wakijisalimisha ambao walikuwa wameletwa na serikali ya Congo kusaidia jeshi katika vita. Taarifa zinasema kuwa raia hao wa Romania walikuwa wanalipwa mara 50 zaidi ya wanajeshi raia wa Congo.

Tuna uwezo wetu wenyewe wa kujadili matatizo yetu na kupata suluhu wenyewe. Mataifa kutoka nje kuja kutupa suluhu ni njia moja ya kupora raslimali zetu,” anasema Mutsuva.

Tulifikaje hapa?

Kuongezeka kwa mapigano hivi karibuni kati ya wanajeshi wa Congo na waasi wa M23 tangu Disemba 2024 kumesababisha vifo vya maelfu ya raia na kuwaacha watu zaidi ya 500,000 bila makazi, kulingana na Umoja wa Mataifa.

DRC na Umoja wa Mataifa wanaishtumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi, madai ambayo Rwanda inakanusha. Waasi wanadhibiti maeneo mengi zaidi na sasa wako Goma na Bukavu—miji miwili mikubwa katika eneo hilo.

Kuongezeka kwa machafuko kulifanya Umoja wa Mataifa kutoa onyo la hatari ya kuwepo kwa vita zaidi katika kanda hiyo. Wanajeshi kutoka mataifa saba ambao waliletwa kusaidia Congo kupata amani walishindwa kufanya hivyo.

Juhudi za majadiliano kadhaa, ikiwemo mpango ulioongozwa na Umoja wa Afrika, pia ulishindwa kusitisha mapigano. Makubaliano ya awali ya kati ya mataifa hayo mawili ya Afrika ya Kati yamesambaratika kutokana na nchi hizo kutoaminiana.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us