Uganda imesema siku ya Jumatatu kwamba ilimkamata mshukiwa mkuu utekwaji nyara wa 2019 wa mtalii wa Marekani na dereva wake katika Mbuga ya Kitaifa ya Queen Elizabeth.
Kimberly Sue Endicott na dereva wake wa Uganda walitekwa nyara Aprili 2, 2019 na watu wenye silaha ambao baadaye walitaka fidia ya $500,000.
Waliachiliwa siku nne baadaye kufuatia mazungumzo yaliyohusisha maafisa wa Uganda na Marekani.
Haijathibitishwa wazi iwapo fidia hiyo ililipwa.
"Vikosi vya usalama vya pamoja hatimaye vilimpata mshukiwa mkuu, Derrick Memory, ambaye amekuwa akitoroka tangu 2019," msemaji wa jeshi Meja Kiconco Tabaro aliliambia Shirika la Habari la AFP.
Memory alikuwa amejificha mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo "ambako alihusika katika vitendo vyngine vya uhalifu," Tabaro alisema.
Uganda ilikuwa ikimfuatilia mshukiwa huyo na hatimae kumkamata katika wilaya ya magharibi ya Kanungu Mei 4, aliongeza.
"Haya ni mafanikio makubwa," Tabaro alisema, akiongeza kuwa mamlaka imedhamiria "kuwahakikishia watalii na umma kwamba Uganda iko salama na wale wanaopanga kuyumbisha nchi yetu watapatikana na kushughulikiwa kwa uthabiti."
Polisi walimkamata mshukiwa mwengine, Onesmus Byaruhanga, wakati huo akiwa na umri wa miaka 43, wakati wa uchunguzi wa awali mwaka 2019 kwa madai ya kuwasaidia watekaji nyara.
Kwa sasa anakabiliwa na mashtaka ya utekaji nyara na wizi wa mabavu.