Mahakama ya nchini Nigeria, imemhukumu adhabu ya kunyongwa Peter Nwachukwu, kwa kosa la kumuua msanii nyota wa muziki wa Injili nchini humo Osinachi Nwachukwu.
Mahakama hiyo ilitoa adhabu ya kunyongwa kwa Peter Nwachukwu ambaye alikuwa ni mume wa msanii huyo, baada ya kumkuta na hatia ya kumuua Osinachi, katika tukio lililotokea Aprili 8, 2022.
Upande wa waendesha mashitaka ulipokea vielelezo kutoka kwa mashahidi 17, wakiwemo watoto wa Osinachi mwenyewe.
Mahakama hiyo ilimkuta Peter Nwachukwu na makosa 23, yakiwemo mauaji ya kukusudia, ukatili dhidi ya mke na unyama kwa watoto.
Kulingana na mahakama hiyo, ushahidi wote ulimusisha Peter Nwachukwu na mauaji hayo.
Mwanamuziki huyo alijizoelea umaarufu kupitia wimbo wake maarufu wa "Ekwueme", alioshirikishwa na Prospa Ochimana.