MAISHA
2 dk kusoma
Fiston Kalala Mayele: Mshambuliaji anayetetemesha Afrika
Mshambuliaji huyu Fiston Kalala Mayele alizaliwa katika mji wa Mbuji-Mayi zamani ukijulikana kama Bakwanga katika mkoa wa Kasai-Oriental ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo miaka 30 iliopita.
Fiston Kalala Mayele: Mshambuliaji anayetetemesha Afrika
Fiston Kalala Mayele. /Reuters
5 Mei 2025

Mfumania nyavu huyu ameshiriki kwenye Ligi Kuu ya DRC inayojulikana zaidi kama Linafoot, akizichezea klabu tofauti zikiwemo AS Simba, na AS Vita Club.

Amekuwa mwiba kila anapokwenda na haichukui muda kwa yeye kuonesha makali yake pindi anapotua kwenye timu mpya.

Yanga ya Tanzania

Nyota ya Mayele ilizidi kung’aa alipojiunga na Dar Young Africans ya Tanzania mwaka 2021, ambako ndani ya misimu miwili, alijizolea umaarufu kwa uhodari wake wa kupachika mabao, lakini zaidi kwa aina ya ushangiliaji wake, ambao ulikuwa gumzo kwa kila rika.

Mayele anapofunga bao anatetemesha mabega yake, ishara ya kufurahia ushindi huo na mara nyingi wachezaji wenzake walikuwa wakiungana naye katika kusherehekea kwa mtindo huo. Na ndipo alipofahamika kama mzee wa kutetema.

Ilikuwa ni burudani tosha kwa mashabiki wa Yanga lakini pia kwa watangazaji wa mpira ambao walipendelea mbwembwe hizo za Mayele anapokuwa uwanjani.

Mashabiki katika kufurahia hilo baadhi wakisema ‘‘matokeo hata yawe mazuri vipi, hayanogi bila Mayele kutetema’’, wakiwa na maana mshambuliaji huyo apate japo goli moja ambalo litawafanya wachangamke kwa kutetema uwanjani.

Mayele aliondoka Jangwani akiwa tayari ametupia magoli 50 kwenye michezo tofauti.

Pyramids FC ya Misri

 Akikipiga na Pyramids ya nchini Misri toka mwaka 2023, tayari Mayele ameshafanya makubwa kwenye ardhi ya mafarao.

Ni hivi majuzi tu, mzee wa kutetema alitupia mabao mawili kati ya matatu, wakati Pyramids ilipoichapa Orlando Pirates katika mchezo wa Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa, na hivyo kumhakikishia mzee wa kutetema nafasi ya kukutana na Mamelodi Sundowns kwenye mchezo wa fainali baadaye mwezi Mei.

Ikumbukwe kuwa, hii haitokuwa mara ya kwanza kwa mtetemaji huyo kufikia hatua ya fainali ya michuano mikubwa barani Afrika.

Kwa ngazi ya klabu, akiwa amefanya katika msimu wa 2022/2023 kwenye Kombe la Shirikisho, akiwa ndani ya uzi wa Young Africans, dhidi ya USM Alger ya Algeria, ambapo USM Alger waliibuka kidedea.

Vile vile, Mayele anajongea fainali hizo akiwa mmoja ya wafungaji bora, baada ya kutia kimiani mabao matano, akilingana na mchezaji mwenzake wa Pyramids Ibrahim Adel, na Emam Ashour wa Al Ahly. Al Ahly tayari wameyaaga mashindano hayo.

Hata hivyo, huenda majeraha yakamuweka nje Ibrahim Adel kwenye mechi mbili za fainali.

Je, hii itakuwa ni fursa ya mzee wa kutetema kutwaa kiatu cha dhahabu?

 

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us