Hawa ndio makinda waliopata kuvuma kwenye historia ya Kombe la Dunia hadi sasa
Hawa ndio makinda waliopata kuvuma kwenye historia ya Kombe la Dunia hadi sasa
Ulikuwa unafanya nini ulipokuwa na umri wa miaka 17? Unadhani wachezaji wengi wa soka huanza kucheza wakiwa na wastani wa umri gani? Kuna baadhi ya wachezaji waliopata mafanikio uwanjani wakiwa na umri mdogo.
21 Machi 2025

Pele

Mmoja ya wachezaji walioweka historia katika mashindano ya Kombe la Dunia na walioanza kutikisa nyavu wakiwa bado wadogo ni pamoja na Pele.

Edson Arantes do Nascimento, maarufu Pele wa Brazil ndiye mchezaji mdogo zaidi katika historia kufunga kwenye mechi ya Kombe la Dunia. Historia inamtambua kama mchezaji pekee mwenye umri wa chini ya miaka 18 ‘kutupia nyavuni’ katika mashindano hayo makubwa ulimwenguni.

Pele aliwafungia ‘Seleção’ jumla ya magoli sita, huku akiisaidia timu yake ya taifa kutwaa Kombe la Dunia mwaka 1958, katika fainali zilizofanyika nchini Sweden.

Wakati huo, Pele alikuwa na miaka 17 na siku 239, na ilikuwa kwenye mechi ya robo fainali kati ya Brazil na Wales, na aliipatia timu yake goli la pekee katika dakika ya 66, na kuiwezesha ‘Selecao’ kusonga mbele.

Kwenye hatua ya nusu fainali, Pele aliifungia timu yake ‘hat-trick’ dhidi ya timu ya taifa ya Ufaransa.

Kwenye fainali dhidi ya wenyeji Sweden akatunisha kapu lake la magoli, kwa kutupia mawili na kufanya matokeo yasomeke 5-2.

Mwaka huo 1958 wacheza samba walinyanyua Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza na kijana mdogo akawa ametambulishwa kwa dunia kutokana na uhodari wake wa kucheka na nyavu.

Manuel Rosas

Mchezaji wa safu ya ulinzi wa Mexico Manuel Rosas Sanchez alizaliwa 17 Aprili 1912. Aliipatia timu yake magoli mawili katika mechi ambayo walishindwa na
Argentina 6-3. Wakati akifunga magoli hayo 1930 Manuel Rosas alikuwa na umri wa
miaka 18 na siku 93.

Siku tatu kabla ya hapo pia aliweka historia ya kuwa mchezaji wa kwanza ‘kujifunga goli’ katika Kombe la Dunia, kwenye mechi yao dhidi ya Chile.

Pia alikuwa mchezaji wa kwanza kufunga penati kwenye michuano ya Kombe la Dunia. Fainali za Kombe la Dunia zilifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1930.

Gavi

Pablo Martin Paez Gavira maarufu Gavi wa Uhispania alipata nafasi hiyo wakati alipoipatia timu yake ya ‘La Roja’ goli katika mechi yao ya Kombe la Dunia dhidi ya Costa Rica. Mwaka 2022 nchini Qatar, Gavi alikuwa na umri wa miaka 18 na siku 110. Walipata ushindi wa magoli 7-0 dhidi ya ‘Los Ticos’. Huu ukiwa ni ushindi mkubwa zaidi katika historia ya michuano hiyo.

Michael Owen

Michael Owen aliifungia timu yake ya ‘Simba Watatu’ wa Uingereza goli katika mechi yao dhidi ya Romania kwenye michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1998, yaliyofanyika nchini Ufaransa. Owen, wakati huo akiichezea Liverpool alikuwa na umri wa miaka 18 na siku 190.

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us