Wakati jukwaa la tano la uchumi la Qatar (QEF 2025) lilipoanza Doha siku ya Jumanne, ziara ya Rais wa Marekani Donald Trump ya hivi punde katika eneo la ghuba bado ni gumzo—siyo tu mijadala kuhusu sera, lakini pia katika masuala ya uwekezaji kimkakati katika kanda na ushirikiano duniani.
Siku chache baada ya Ikulu ya Marekani kudai kuwa imefanikiwa kupata uwekezaji wa zaidi ya trilioni 2 kutoka mataifa ya Ghuba, QEF 2025 limekuwa jukwaa ambapo viongozi wa sekta ya fedha,watunga sera, na wajisiriamali wanajaribu kufanya kudadavua hili linamaanisha nini —na kama nchi za Ghuba zinaegemea upande wa Marekani katika kipindi ambacho kuna mvuta kati ya mataifa ya Mashariki na Magharibi.
Miongoni mwa masuala yanayozua mijadala ni zawadi ya ndege kutoka kwa Qatar aina ya Boeing 747-8 yenye thamani ya dola milioni 400 – iliyoitwa “kasri la hewani” – kuchukua nafasi ya ndege ya Air Force One ambayo ni zamani — hatua ambayo imezua hasira kwa wawakilishi wa chama cha Democratic, na kufurahiwa na Trump mwenyewe.
Huku Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani akitetea hatua hiyo kama “jambo la kawaida linalofanyika kati ya washirika,” Kiongozi wa Seneti wa chama cha Democratic Chuck Schumer aliwasilisha sheria ya kupiga marufuku ndege ya kigeni kutumika kama ndege ya rais, akionya kuhusu ‘ushawishi kutoka’ mataifa ya nje.
Lakini Qatar inaonesha kutojali kuhusu hilo.
"Tunatakiwa kuondokana na hali hii,” Waziri Mkuu Al Thani alisema wakatik wa ufunguzi wa jukwaa hilo. “Sijui kwa nini watu wanadhani kuwa hii ni rushwa au Qatar kujaribu kununua ushawishi. Hili ni jambo la kawaida kati ya mataifa.”
Mfuko wa uwekezaji wa Qatar siyo tu kuhusu masuala ya diplomasia — inasisitiza suala la dola.Afisa Mkuu Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Qatar (QIA) Mohammed Al Sowaidi ametangaza uwekezaji zaidi: dola bilioni 500 Marekani katika muongo mmoja ujao, wakiangazia Akili Mnemba, huduma ya afya, na vituo vya kukusanya data.
“Tunaamini katika ukuaji na uwezo wa mfumo wa Marekani,” Al Sowaidi alisema.
Taarifa hizi hazikuwa tu mazungumzo. Wiki iliyopita tu, wakati wa ziara ya Trump ya maeneo ya Ghuba, Boeing ilisaini mkataba mkubwa na shirika la ndege la Qatar Airways wa kununua ndege 160, na uwezekano wa kununua 50 zaidi.
Kwa jukwaa lililoanzishwa kwa misingi ya majadiliano, suala hilo lilikuwa na maana pana.
Mataifa yenye uchumi unaokuwa, wajasiriamali yatoa wito wa ushirikiano zaidi
Marekani inaangazia tu yaliyojiri katika siku ya kwanza ya ufunguzi wa jukwaa hili la QEF, ambapo sauti za mataifa ambayo uchumi unakuwa, wajasiriamali, na wabunifu wametoa wito wa kuwepo mizania, ushirikiano ulimwenguni — hali ambayo inasaidia masoko yanayokuwa badala ya kuyaweka pamoja na mashirika hasimu.
Thomas Hopper, Mwenyekiti wa Die Jungen Unternehmer yenye makao yake Berlin (ikimaanisha Wajasiriamali Vijana), alitoa mtazamo wa Ulaya ulio na msingi. “Ujerumani imeona miaka mitatu ya kushuka kwa uchumi,” aliambia TRT World.
“Lakini kinachonirudisha QEF ni fursa inayoleta ya kujenga kitu kipya kupitia ushirikiano, si ushindani. Eneo hili, hasa Qatar, linaibuka kama kichocheo cha ujasiriamali wa kimataifa,” alisema mjasiriamali huyo wa Kijerumani.
Hisia za Hopper ziliungwa mkono na Fahad Garba Aliyu, Mshirika Mkuu wa Ignite Capital ya Nigeria, ambaye alisisitiza umuhimu wa mhimili wa ukuaji wa “Kusini kwa Kusini.”
“Afrika ina idadi ya watu wachanga zaidi na uchumi unaokua kwa kasi zaidi. Ghuba ina mtaji na ukaribu. Tuko hapa kuchunguza jinsi tunavyoweza kushirikiana,” Aliyu alisema. “Wakati Magharibi inajiondoa, ni wakati wa Kusini mwa Dunia kufikia uwezo wake kamili.”
Kati ya uvumbuzi wa Akili Mnemba na hali halisi za siasa ulimwenguni
Wakati siasa za kimataifa zilitupa kivuli kizito, tukio hilo pia lilionyesha uvumbuzi wa ndani na mabadiliko ya kidijitali.
Susanna Ingalls, mwanzilishi mwenza na Afisa Mkuu wa Bidhaa katika Urban Point, jukwaa lenye makao yake Doha, anaamini kuwa majukwaa kama QEF yanasaidia biashara ndogo ndogo kuendelea kuunganishwa na mwelekeo wa makro unaobadilika.
“Tunapitia mabadiliko ya Akili Bandia sisi wenyewe,” alisema mjasiriamali huyo wa Marekani ambaye amefanya Doha kuwa nyumbani kwake kwa muongo mmoja uliopita. “Ni jambo la kusisimua lakini pia la kutisha. Maendeleo tunayoyaona kila mwezi ni ya kushangaza. Na nadhani Doha—kwa tabia yake ya kimataifa—imewekwa vyema kama kitovu cha uvumbuzi wa kimataifa.”
Alipoulizwa kuelezea uchumi wa dunia kwa neno moja, Ingalls alijibu: “Uunganisho.”
“Hata uwepo wa Trump hapa hivi karibuni,” aliongeza, “unaashiria umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa. Sikubaliani na sera zake zote, lakini kama mfanyabiashara, anajua thamani ya amani na utulivu. Na hilo lina athari kubwa kwa vipaumbele vya kiuchumi.”
Mashindano ya Marekani na China yanajitokeza kama mvutano
Licha ya ushiriki wa hali ya juu wa Trump, hali nyingine ilijitokeza pembezoni mwa mazungumzo: mashindano ya kudumu kati ya Washington na Beijing kwa ushawishi wa kimataifa.
Abdulaziz Said Humaid Al Risi, Naibu Rais wa Chuo cha Usimamizi cha Oman, alisisitiza hali hii ya uwiano muhimu.
“Mvutano kati ya Marekani na China kimsingi ni kuhusu mataifa haya mawili kujaribu kupata faida katika biashara ya kimataifa na siasa za kijiografia,” aliambia TRT World. “Kwetu sisi katika Ghuba, hili linatoa changamoto na fursa. Nchi kama Oman lazima ziendelee kuwa na uhusiano thabiti na wenye uwiano na China na Marekani,” aliongeza.
“Uchumi hizi mbili zinaunda mazingira ya kiuchumi ya dunia, na ni muhimu tusikose fursa yoyote inayoweza kutokea kutokana na ushirikiano na upande wowote,” alisema, akielezea jinsi jukwaa hili linavyothibitisha fikira za Ghuba kimkakati.
Al Risi pia alielezea mvutano wa kikanda kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa hali kati ya India na Pakistan na vita vinavyoendelea vya Israeli dhidi ya Gaza, akionya kuwa hali hizi za kutokuwa na uhakika zinatishia “utulivu wa kiuchumi kote katika eneo hilo na duniani.”
Siku ya kwanza ya QEF inaweza kukumbukwa kwa habari kuhusu ndege ya Trump iliyotolewa kama zawadi na majibu ya hasira yaliyoibuka. Lakini kwa undani, jukwaa linatoa ujumbe wa kina zaidi na wenye maana: Ghuba—na Doha hasa—inatamani kujikita kama mhimili kati ya nguvu zinazoshindana, kama kitovu cha vipaji, mtaji, na mawazo katika dunia inayozidi kugawanyika.
Kwa viongozi wa Ghuba na wenzao kote Kusini mwa Dunia, swali si kuchagua upande bali ni kubaki muhimu kwa pande zote mbili. Hilo linaweza kuwa rasilimali kubwa zaidi kidiplomasia na kiuchumi kwa Qatar.