Umuhimu wa Hijja kwa Muislamu
ULIMWENGU
4 dk kusoma
Umuhimu wa Hijja kwa MuislamuHijja ni nguzo ya tano ya Kiislamu, ni wajibu kwa mtu ambaye ana uwezo wa kiafya na kifedha kuhiji angalau mara moja katika maisha yake.
Waislamu wameanza kumiminika mji mtukufu wa Makka, Saudi Arabia, kwa ajili ya ibada ya Hajj. / Reuters
21 Mei 2025

Hijja ni moja ya nguzo tano za Uislamu na ibada ya kipekee inayokusanya ibada mbalimbali kama vile swala, toba, sadaka, subira, na mshikamano wa Kiislamu.

Mwaka wa 2025 unatoa fursa nyingine muhimu kwa Waislamu kutoka kila pembe ya dunia kujumuika katika ardhi takatifu ya Makka iliyopo nchini Saudi Arabia, kutekeleza ibada ya Hijja kwa ajili ya kutafuta radhi ya Mwenyezi Mungu.

Ibada hii hufanyika katika mwezi wa Dhul-Hijja, mwezi wa mwisho katika kalenda ya Kiislamu.

Hijja ni ibada ambayo ni lazima kwa Waislamu waliokidhi masharti ya kiafya, kifedha, na usalama wa safari.

Katika Qur’an Tukufu, Mwenyezi Mungu anasema: “Na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ni wajibu kwa watu kuhiji Nyumba hiyo – kwa mwenye uwezo wa kufunga safari...” (Surat Al Imran, 3:97)

Hii ni amri ya wazi inayoweka Hijja kuwa jukumu la lazima kwa kila Muislamu mwenye uwezo wa kimwili na kifedha. Hii inaonyesha kuwa Hijja si jambo la hiari, bali ni wajibu wa moja kwa moja.

Hija ni safari ya toba, msamaha na kujikurubisha kwa Mola. Inawakumbusha Waislamu juu ya usawa wa binadamu, unyenyekevu na mshikamano wa Ummah wa Kiislamu. Katika vazi la Ihram (shuka leupe inalovaliwa na wanaume), tajiri na masikini, mweupe na mweusi, wote husimama mbele ya Allah wakiwa sawa.

Kwa waumini wa Afrika Mashariki, kutoka Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda na Burundi, Hijja ni ibada yenye umuhimu mkubwa kiroho lakini pia inahitaji maandalizi makubwa ya kifedha, afya na usafiri.

Hijja na kusafishwa kwa dhambi

Kwa mwaka huu wa 2025, waumini wanaotegemea kwenda Hijja wanapaswa kuelewa kuwa Hijja sahihi ni kama kuanza upya maisha. Mtume Muhammad (Rehema na Amani Ziwe Juu Yake) amesema:

"Yeyote afanyaye Hijja na asiseme maneno machafu, wala asifanye maasi (madhambi), atarejea nyumbani akiwa kama siku alipozaliwa na mama yake." (Hadithi sahihi – Imepokewa na Bukhari na Muslim)

Hii ina maana kwamba Hijja ni njia ya kusamehewa madhambi yote ya nyuma, na ni neema kubwa ya kiroho inayopatikana kwa mtu mmoja mmoja pekee.

Katika Hijja, mamilioni ya Waislamu kutoka mataifa, rangi, na lugha tofauti hukusanyika kwa ajili ya lengo moja: kumuabudu Mwenyezi Mungu. Hili linaimarisha mshikamano wa Kiislamu na kuvunja mipaka ya kijamii, kikabila, na kitaifa.

Mabadiliko ya Hijja mwaka 2025

Mwaka huu wa 2025, Hijja imepangwa kufanyika kati ya Juni 4 hadi Juni 9. Kuna mabadiliko kadhaa yaliyowekwa na Serikali ya Saudi Arabia:

Mabadiliko ya bei na idadi maalum ya watu

Nchi kadhaa, hasa zile za Afrika, zimeathiriwa na kushuka kwa thamani ya sarafu, jambo lililoongeza gharama za Hijja. Nchini Ethiopia, kwa mfano, gharama zimeongezeka kwa zaidi ya asilimia 90.

Hapo awali, gharama kwa Waislamu wa Ethiopia kuhiji ilikuwa birr 329,000 sawa na dola 4,921 za Marekani. Walakini, mwaka huu, imeongezeka hadi 625,000 birr sawa na dola 5,026 za Marekani .

Katika mkutano na waandishi wa habari tarehe 11 Februari, 2025, viongozi wa baraza kuu la Sekta ya Hijja, walihusisha ongezeko hili, kwa sehemu, na kushuka kwa thamani ya sarafu ya nchi hiyo dhidi ya dola ya Marekani.

"Pamoja na jitihada kubwa za baraza la kuoanisha gharama za usafiri wa Hijja na uwezo wa kifedha wa umma, kushuka kwa thamani ya sarafu ya Ethiopia na ukweli kwamba ada zote za huduma zinalipwa kwa fedha za kigeni zimechangia gharama kubwa," alifafanua Sheikh Abdulaziz Sheikh Abdul Woli, Makamu wa Rais wa Baraza Kuu na Mkuu wa Sekta ya Hija na Umra.

Inatarajiwa kuwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki zitakumbwa na changamoto kama hiyo.

“Nchini Kenya, idadi ya watu waliopangiwa kufanya ibada ya Hijja mwaka huu ni takriban 4,300. Gharama za safari ya Hijja zinaanzia dola 4,500 za Marekani hadi kufikia dola 5,500. Hata hivyo, kwa wale waliochelewa kutafuta huduma hizo, baadhi wamejikuta wakilipa hadi takriban dola 7,000”, anaeleza Hamza Mukhtar.

Ikilinganishwa na mwaka jana, gharama ilikuwa karibu dola 4,000.

Mukhtar, ambaye anaongoza ofisi ya mawakala wa kusafirisha Waislamu kwenda Makka kwa ibada ya Hijja na Umra, anasema kuwa tofauti na miaka ya nyuma, mwaka huu visa za Hijja zilitolewa mapema, hali itakayowezesha asilimia kubwa ya mahujaji wa Kenya kuondoka kwa wakati.

Kwa upande wa usalama na nidhamu, idara ya kushughulikia wageni wa mji mtukufu wa Makka imeimarisha hatua za kiusalama.

“Hatua hizo zimewekwa kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayevuka mipaka ya kufanya ibada ya Hijja bila kibali rasmi cha ‘Nusuk’, kibali ambacho kina kodi ya ‘QR’ inayotumika kumtambua mgeni iwapo amesajiliwa kwa ibada hiyo au la. Hii imelenga kudhibiti msongamano wa watu”, ameongeza Mukhtar.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us