Pierre-Emerick Aubameyang alifunga mabao mawili Gabon ilipoibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Kenya katika mechi yao ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2026 jijini Nairobi Jumapili na kusogeza Gabon alama mbili juu ya Côte d'Ivoire katika kinyang'anyiro cha kuwania kufuzu kwa fainali nchini Marekani, Mexico na Canada.
Gabon, ambayo haijawahi kufuzu kwa Kombe la Dunia, inasonga mbele hadi pointi 15 baada ya mechi sita katika Kundi F, huku Côte d'Ivoire ikiwa na pointi 13 kutokana na mechi tano na wanasafiri ugenini Gambia Jumatatu.
Timu inayoongoza katika kila kundi kati ya makundi tisa hupata nafasi ya kufuzu, huku washindi wa pili, wanne wakiingia katika kampeni ngumu ya mchujo baina ya mabara kwa mchujo mmoja zaidi.
Aubameyang, 35, alifunga bao lake la kwanza kwa umaliziaji mzuri kutoka umbali wa mita 15 na kupenya mikono ya kipa, kabla ya kuongeza la pili kwa mkwaju wa penalti kufuatia mpira wa mkono kwenye eneo la hatari.
Kenya inatishiwa kubanduliwa
Huenda Kenya sasa wako nje ya mchujo wakiwa na pointi sita kutokana na mechi sita. Walirudisha bao kupitia kwa Michael Olunga lakini kocha mkuu mpya Benni McCarthy amefanikiwa kupata pointi moja katika mechi zake mbili za kwanza akiwa kocha.
Katika mechi nyingine pekee Jumapili, Eswatini na Mauritius walitoka sare ya 3-3 iliyochezewa nchini Afrika Kusini. Wote wawili hawana matumaini ya kufuzu Kombe la Dunia.